The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Vigogo Chadema, Wakili wa Serikali Acharuka

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku moja kwa mawakili wa pande zote mbili katika kesi inayowakabili vigogo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujadiliana kisheria na kuwasilisha hoja zao ili waanze kujitetea.

 

Vigogo hao tisa wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi, akiwamo Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, wanashtakiwa kwa mashtaka 13 ya uchochezi.

 

Jana, wakili wa utetezi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, anayesikiliza kesi hiyo kwamba kesi imepangwa kusikikiza ushahidi wa utetezi na walikuwa na shahidi mmoja.

 

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi, alipinga shahidi wa nje kusikilizwa ushahidi wake kabla washtakiwa hawajajitetea kwa sababu utaratibu huo unakinzana kisheria.

 

“Mheshimiwa Hakimu kuna changamoto kubwa mahakama yako kuanza kuwasikiliza mashahidi wa nje kabla washtakiwa hawajajitetea. Utaratibu huo unakinzana na sheria upande wa Jamhuri unaupinga,” alidai Nchimbi.

 

Hakimu Simba aliamuru pande zote mbili zikapitie na kusoma sheria ili wawasilishe hoja za pingamizi hilo la awali na majibu.

 

Alisema kesi hiyo itaendelea kesho mahakamani hapo kusikiliza hoja za kisheria za mawakili.
Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu Dk. Vicent Mashinji; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

 

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 likiwamo la kula njama wakiwadaiwa kuwa Februari 1 na 16, mwaka jana, jijini Dar es Salaam, walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyika.

Comments are closed.