The House of Favourite Newspapers

Khalid Aucho Azua Hofu Yanga Madaktari Kumfanyia Vipimo Vya Afya

0
 Khalid Aucho,

KIUNGO wa Yanga, Khalid Aucho, amezua hofu kikosini hapo baada ya kupata majeraha, huku jopo la madaktari wa timu hiyo, linatarajiwa kumfanyia vipimo vya afya kufahamu ukubwa wa jeraha lake.

Kiungo huyo raia wa Uganda, juzi Jumapili alishindwa kumaliza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Real Bamako uliochezwa nchini Mali baada ya kupata majeraha ya goti na kutolewa uwanjani kipindi cha kwanza.

Mganda huyo baada ya kutolewa, nafasi yake ilichukuliwa na Mburkinabe, Stephane Aziz Ki ambaye alipiga asisti ya bao la Yanga lililofungwa na Mkongomani, Fiston Mayele. Mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kiungo huyo leo Jumanne anatarajiwa kufanyiwa vipimo hivyo, licha ya kupatiwa huduma ya kwanza wakiwa Mali.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo alipata majeraha ya goti ambayo yalimfanya ashindwe kuendelea na mchezo huo.

Aliongeza kuwa vipimo vya afya atakavyopatiwa ndivyo vitaamua hatima yake wakati timu hiyo ikiwa na michezo muhimu na migumu ya kimataifa ya marudiano dhidi ya US Monastir na Real Bamako nyumbani, kisha ugenini dhidi ya TP Mazembe.

“Hatma ya ukubwa wa majeraha ya Aucho, yatajulikana mara baada ya timu kurejea nyumbani leo (jana Jumatatu) ikitokea Mali ilipokwenda kucheza dhidi ya Bamako.

“Majeraha hayo yalimfanya ashindwe kuendelea na mchezo kabla ya kutolewa kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza hapo uwanjani.

“Hivyo mara baada ya timu kurejea Dar, haraka atafanyiwa vipimo vya afya chini ya jopo la madaktari wa timu yetu ili kuhakikisha anarejea haraka uwanjani kuipambania timu yake,” alisema mtoa taarifa huyo.

STORI NA WILBERT MOLANDI

#EXCLUSIVE: SALEH JEMBE AFICHUA MPASUKO SIMBA, SARE ya YANGA – ”MANGUNGU HAWEZI KUWA YANGA”…

Leave A Reply