The House of Favourite Newspapers

MTV Mama: Kiba Vs Diamond, Derby Nyingine Sauz Leo

kiba-diamond

Makala: Erick Evarist

PICHA lilianza kwenye shoo ya Mombasa, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ alipokuwa akikamua jukwaa moja na msanii wa Kimataifa kutoka Marekani, Chris Brown.

Kitendo cha meneja wa Diamond, Sallam Sharaf kuwepo kwenye shoo ile kiliibua utata  baada ya Kiba kuzimiwa kinasa sauti ‘mic’. Kiba alilaumu uwepo wa Sallam. Mitandaoni kukawaka moto.

mama1Bifu la Kiba na Diamond (Nasibu Abdul) likazidi kukolea. Kiba alienda mbele zaidi kwa kuhoji hata kama hawana bifu na Diamond lakini meneja  wake alifuata nini pale? Walakini huo! Wajuzi wa mambo mitandaoni wakaitafsiri kauli hiyo kwamba ina shabihiana na ‘hujuma’ aliyofanyiwa kwenye shoo hiyo hadi kuzimiwa mic.

Sallam akamkataa Kiba, akamwambia yeye hahusiki na jambo hilo. Akamtaka Kiba awaeleze ukweli mashabiki wake nini kilitokea kuliko kuwa na kasumba ya kumsingizia yeye au Diamond pindi anapoharibu kitu.

diamondNyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’.

Kwa kumuongezea, Sallam alimwambia Kiba yeye alikwenda pale kwa shughuli zake na ndivyo wafanyavyo mameneja  wengi na wasanii kwenda kujifunza katika shoo za wasanii wengine hata kama wao hawahusiki na shoo husika.

Akamwambia ajiandae maana kama ni suala la yeye kukutana naye katika shughuli moja, wangekutana tena kwenye African Muziki Magazine Awards (Afrimma) zilizofanyika nchini Marekani wikiendi iliyopita.

alikiba Nyota wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’.

Kwenye tuzo, mahasimu Diamond na Kiba walikuwa wakichuana katika kipengele kimoja cha msanii Bora wa Afrika Mashariki, Diamond akaibuka kidedea kwa kumgaragaza Kiba na wasanii wengine wa Afrika Mashariki kama Eddy Kenzo, Jose Chamilione na Bebe Cool.

Baada ya ushindi huo, uliibuka tena mjadala kutoka kwa wafuasi wa Kiba, kwamba kruu la Diamond (WCB) huwa halishindi kihalali. Wamekuwa wakinunua tuzo mara kwa mara na ndiyo maana hata tuzo hizo, kijana anayechipukia katika lebo yao, Harmonize naye aliweza kujinyakulia tuzo ya Msanii Bora Chipukizi.

Bwa’mdogo huyo aliwagaragaza Nathi wa Afrika Kusini, Locko wa Cameroon na wengineo. Lakini kutokana na dhana  ambayo inaaminika kuwa Kiba amekuwa akiwatuhumu kuwa wananunua tuzo hizo, Babu Tale ambaye ni mmoja wa mameneja wa Diamond aliibuka mapema wiki hii na kusema kama kununua ni rahisi basi na wao wanunue.

Bifu la Diamond na Kiba linakolea sana Kibongobongo kutokana na kila shabiki wa pande hizo kutaka kumpa ufalme msanii wake. Upande wa Diamond wanaamini Diamond ndiye mfalme lakini ule wa kina Kiba unaamini Kiba ana uwezo mkubwa, ana sauti nzuri na kamwe Diamond hawezi kumfikia.

Wakati mtifuano wa ufalme ukiendelea, miamba hiyo miwili inakutana tena leo nchini Afrika Kusini katika MTV African Music Awards (Mama). Unaweza kuiita ni Derby nyingine!

Mashabiki wa miamba hiyo wana kimuhemuhe cha kuona nani anaibuka kidedea katika vipengele tofauti vya tuzo hizo. Kiba amependekezwa kwenye vipengele viwili tofauti; Wimbo Bora wa Kushirikishwa (Unconditionally Bae) pamoja na Wimbo Bora wa Mwaka ambao ni  Unconditionally Bae alioshirikiana na Sauti Sol wa Kenya.

Kiba ana changamoto zake. Katika kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikishwa wanachuana na wakali; Mnaigeria, Patoranking Ft Sarkodie – (No Kissing), Msauz, Nasty C Ft Davido, Cassper – (Juice Back-Remix), Msauz, AKA Ft Burna Boy, Khuli Chana & Yanga – (Baddest) na Msauz, DJ Maphorisa Ft Wizkid & Dj Bucks – (Soweto Baby).

Kwa upande wa Diamond, amependekezwa katika vipengele vya Msanii Bora wa Mwaka na Msanii Bora wa Kiume. Kibarua chake si cha kitoto maana kwenye Msanii Bora anachuana na AKA, Patoranking, Wizkid na Black Coffee ambaye alimmwaga vibaya katika BET Awards, mwaka huu.

Tusikilizie matokeo!

Comments are closed.