The House of Favourite Newspapers

Kichuya: Hakyanani Yanga Wangekula Tatu

kichuya-simba3

Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam
BAADA ya kuisawazishia timu yake dakika za lala salama, kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, amewaambia watani wao wa jadi Yanga kama isingekuwa kadi nyekundu ya Jonas Mkude, basi wangewafunga mabao siyo chini ya matatu.

Kauli hiyo, aliitoa jana mara baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara kumalizika kwa timu hizo kutoa sare ya bao 1-1, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

simba

Wachezaji wa Simba wakiwa katika mzozo na refa.

Katika mechi hiyo, Simba ndio waliosawazisha kupitia kwa Kichuya kwa kona iliyoingia moja kwa moja dakika ya 87 ya mchezo huo huku lile la Yanga likifungwa na Mrundi, Amissi Tambwe.

Akizungumza na Champoini Jumatatu, Kichuya alisema katika mechi hiyo, kocha wao Mcameroon, Joseph Omog ndiye anastahili kupongezwa kutokana na maelekezo mazuri aliyowapa kipindi cha mapumziko wakiwa vyumbani.

Kichuya alisema, kocha huyo aliwataka kutuliza presha ya mchezo mara baada ya mwamuzi, Martin Saanya kumtoa kwa kadi nyekundu Mkude katika dakika ya 26 na kuwataka kucheza soka la nidhamu ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kufanikiwa kusawazisha bao hilo.
“Bao hili la kusawazisha nililolifunga mimi liende kwa kocha wetu Omog, kiukweli alifanya kazi vizuri ya kutupa baadhi ya maelekezo wakati wa mapumziko vyumbani.

yanga-simba-3

Mshambuliaji  wa Kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma (katikati) akipambana na wachezaji wa Simba.

“Tukiwa vyumbani, kocha alitutaka kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, pia kutimiza majukumu yetu ya ndani ya uwanja kwa maana ya mabeki kuzuia hatari golini, viungo kuchezesha timu licha ya Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu na washambuliaji kufunga.

yanga-simba-4

Mchezaji wa Yanga akimchezea rafu Ibrahim Ajibu.

“Na ndiyo maana uliona tulivyorudi uwanjani, timu ilibadilika kwa kucheza kwa kujiamini na kulishambulia goli la Yanga kila wakati, lakini nikwambie tu, kama Mkude asingetolewa kwa kadi nyekundu, niamini tungewafunga Yanga mabao matatu kutokana na ubora wa kikosi chetu,” alisema Kichuya.

yanga-simba-2
Aliongeza: “Ujue mimi ndoto na malengo yangu ilikuwa ni lazima niifunge Yanga, kama unavyojua hii ndiyo ‘derby’ yangu ya kwanza mimi kucheza, sasa ninapofunga ni lazima nijisikie furaha, lakini shukrani zangu ziende kwa benchi la ufundi, viongozi kwa kuniamini kunipa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.”
Wiki chache zilizopita kabla ya mchezo huo wa juzi, Kichuya aliliambia gazeti hili kuwa anaisubiri Yanga kwa hamu na kweli amefanikiwa kuifunga.

yanga-simba-1
Wakati huohuo, bao la Kichuya wa Simba dakika za mwisho kwenye matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya watani, Yanga liliweka rekodi mpya kwenye historia ya timu hizo, ikiwa ni sare ya sita katika mechi walizokutana mwezi Oktoba.

Takwimu zinaonyesha kabla ya mchezo huo, timu hizo zilikuwa zimekutana mara 17 kwenye mechi za mwezi Oktoba ambapo Yanga ilikuwa imeshinda mara sita kama Simba, huku zikitoka sare mara tano, hivyo sasa wako ngoma droo.

Aidha, katika michezo 82 waliyokutana kwenye ligi kuu, sare zilikuwa 28, Yanga wameifunga Simba mara 31, huku wao wakifungwa mara 23 tu.

Comments are closed.