TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha mahakamani, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa taasisi hiyo, Bi. Kulthum Ahmed Mansoor, kwa kosa la kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia fedha taslimu kwa njia ya udanganyifu.
Kulthum amefikishwa mahakamani hapo, leo Machi 29, 2019, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Calvin Mhina na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wankyo Simon, na kusomewa mashtaka manane, yakiwemo ya uhujumu uchumi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha zaidi ya shilingi Sh 1,477,243, 000 (bilioni 1.4).
“Uchunguzi uliofanywa ulibaini viwanja vilivyoahidiwa kuuzwa vilikuwa zaidi ya 300, fedha alizolipwa Bi. Kulthum ni zaidi ya Bil. 1 na mil. 400. Mtuhumiwa anadaiwa alijipatia fedha nyingine zaidi ya mil. 200 ambazo alilipwa kama gharama kwa ajili ya hati,” amesema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote huku akinyimwa dhamana kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kesi kuahirishwa hadi Aprili 12, mwaka huu.
Jana Rais Magufuli alielezea tukio hilo na kushangaa kwa nini mtu huyo alikuwa hajapelekwa mahakamani.
“Kuna mkurugenzi mmoja pale makao makuu amewauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake vya zaidi ya shilingi bilioni lakini hajapelekwa mahakamani. Wala sijapata taarifa iwapo hela amezirudisha kwa wafanyakazi aliowadhulumu, kwani wale wafanyakazi wameshindwa kumdai kwa sababu ni bosi wao, wanaumia, wanalalamika pembeni.
“Amewadanganya kwamba ana viwanja kule Bagamoyo, mpaka leo hawajapewa. Najiuliza, Takukuru ni kwa ajili ya watu wengine na sio kwa wao pia? Nataka hili mlishughulikie,” alisema rais.
Na Denis Mtima | Global Publishers
Comments are closed.