The House of Favourite Newspapers

Kijana wa Nyerere, Mbabe wa Idd Amin Atimiza Miaka 100

0

MKUU wa Majeshi mstaafu nchini Tanzania, Jenerali David Musuguri maarufu ‘Chakaza’ au Mtukula,  ametimiza umri wa karne moja (miaka 100) tangu alipozaliwa Januari 4, 1920.

 

Hafla ya kuadhimisha miaka 100 ya Msuguri inafanyika leo Jumamosi Januari 4, 2020 nyumbani kwake kijiji cha Butiama mkoani Mara kwa ibada maalum inayoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila.

 

Mmoja wa wana familia, Bahame Nyanduga, amesema pamoja na ibada, maadhimisho hayo pia yatahusisha shughuli na sherehe za kifamilia. Ibada ya shukrani inayofanyika nyumbani kwa mkuu huyo wa jeshi mstaafu imehudhuriwa na viongozi kadhaa wakiongozwa na Mbunge wa Musoma vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo.

 

Pamoja na ngazi mbalimbali za kijeshi, Msuguri alikuwa Mkuu wa Majeshi kati ya mwaka 1980 hadi 1988. Katika moja ya mahojiano yake,  aliwahi kusema alichukizwa na unyama ambao Idd Amin alikuwa anaufanya na angetokea akamkamata angemchinja.

 

Wakati wa vita ya Kagera,  aliongoza vikosi vya Tanzania kumpiga aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin Dada, mwaka 1979. Msingi wa vita hiyo ilitokana na Amin kuuvamia mkoa wa Kagera, Novemba 1978, hali ambayo rais wa wakati huo, Mwalimu Nyerere hakukubaliana nao na kutangaza kumpiga na kumwondoa.

 

Katika uvamizi huo, Amin alishusha bendera ya Tanzania na kupandisha bendera ya Uganda huku Watanzania ambao hawakuwa na hatia, wakubwa kwa wadogo, waliuawa na wengine kupata vilema vya kudumu, hali ambayo ilimuudhi  Rais wa Tanzania wa wakati huo, hayati Julius Nyerere,  na kutangaza vita ambayo Tanzania ilishinda chini ya Msuguri.

 

Msuguri alisema kwenye uwanja wa vita majeshi ya Amin yalipigwa na majeshi ya Tanzania na kusababisha Ikiongozi huyo kukimbilia Libya alikopewa hifadhi.

Akihubiri wakati wa misa hiyo, Msonganzila amefichua siri ya Msuguri kuishi miaka 100  akisema  ni mazoezi ya kijeshi, nidhamu ya maisha na vyakula vya asili.

 

“Hofu ya Mungu ni siri nyingine iliyomfanya Mzee Msuguri kuishi miaka mingi. Maisha ya amani na heshima kuanzia ndani ya familia, serikalini na jamii kwa ujumla pia ni miongoni mwa sababu za Jenerali Msuguri kuishi miaka 100,” alisema Msoganzila.

 

Mahubiri hayo yalianza kwa kuongoza familia, ndugu, jamaa, marafiki na viongozi kadhaa wa serikali na jamii kumwimbia wimbo wa “happy birthday” ambapo Msonganzila amemwombea Msuguri kuishi miaka mingine 100 na kufikisha miaka 200.

 

Leave A Reply