The House of Favourite Newspapers

Kimei: Serikali Ikakope Nje

0

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei amesema deni la taifa ni himilivu na thamani ya shilingi ni nzuri na Serikali inaweza kutumia kwenda kukopa fedha kwenye soko la dunia kwa riba ndogo ili kukamilisha miradi mikubwa nchini.

 

 

Kimei ametoa kauli hiyo bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha mpango wa tatu wa maendeleo ya kitaifa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/22 – 2025/26.

 

 

Pia ameipongeza Serikali kwa kuuweka uchumi wa nchi kwenye hali ya utulivu na nzuri katika kipindi cha ugonjwa wa Covid-19 na mfumuko wa bei uko chini.

 

 

“Tunaona hali ya deni la taifa ni himilivu na thamani ya shilingi yetu iko nzuri hiyo ni faida kubwa ambayo tunaweza kuitumia kufanya utafiti na kwenda kukopa kwa riba ya chini sana ya asilimia 5 au 6 kwa kukopa moja kwa moja ili tukamilishe ujenzi wa miradi mikubwa tunayoendelea nayo” amesema.

 

 

Amesema hakuna sababu ya kucheleweshwa kwa ujenzi wa miradi mikubwa ya mkakati ikiwemo reli ya kisasa SGR na bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambayo ni chachu kwa ukuaji wa uchumi wanchi.

 

 

“Hakuna sababu ya kuchelewesha wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi mikubwa kama SGR na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere wakati tunaweza kukopa na kukamilisha haraka na kuona matunda kwa miradi hiyo mikubwa ambayo ni chachu katika ukuaji wa taifa letu,” amesema.

 

 

Amesema ni wakati muhimu ambao Serikali inatakiwa itumie kama fursa kwa kwenda kukopa kwenye soko la dunia badala ya kukopa ndani ya nchi kwakuwa wakifanya hivyo watazibana sekta binafsi.

 

 

“ Tusizingatie kukopa ndani kwa sababu tunatakuwa tunaumiza sekta binafsi kwakuwa hawawezi kwenda kukopa nje kwasababu hawajulikani, Serikali inajulikana na kama tukihamasika kwenda kukopa nje na kuacha resources za ndani zikakopwa na watu binafsi kwanza riba zitakuwa chini,” amesema Kimei.

Leave A Reply