The House of Favourite Newspapers

KINGWANGALLA KUFUNGUA ONYESHO LA ‘CHIMBUKO LA BINADAMU’ DAR

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa  Prof. Audax Mabulla, (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Kulia ni Balozi wa  Hispania nchini, Felix Costales.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonyesho ya Chimbuko la Mwanadamu yatakayofanyika katika Makumbusho ya Taifa kesho Januari 23, jijini Dar es Salaam katika Mtaa wa Shaaban Robert.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mtafiti wa Kimataifa Prof. Audax Mabulla, amesema sinema na onyesho hilo ni matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanyika katika bonde la Olduvai na Laetoli, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.

 

Alisema onyesho hilo litaanza kesho saa 11 jioni ambapo wananchi, viongozi na mabalozi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.

Alieleza kuwa zana zote za zimepatikana katika onyesho hilo na vimehifadhiwa ndani ya Makumbusho ya Taifa ambapo miongoni mwake ni masalia ya zamadamu, zana za mawe na masalia ya wanyama walioishi takribani miaka milioni nne iliyopita.

 

“Onesho limegawanyika katika sehemu kuu nne zinazowiana ambapo sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizogunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dkt. Mary D.Leakey. Nyayo hizi ziliachwa na zamadamu anayeitwa Australopithecus afarensis na ni ushahidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopita,” alifafanua.

 

Maonyesho hayo yameandaliwa na Makumbusho ya Taifa ikishirikiana na Ubalozi wa Hispania nchini, Makumbusho ya Akiolojia ya Madrid, Taasisi ya Chimbuko la Binadamu (IDEA) Madrid, Chuo Kikuu cha Alcala Madrid na Makumbusho ya CosmoCaixa Barcelona- Spain na kampuni ya Simenti ya Twiga.

Comments are closed.