The House of Favourite Newspapers

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Agoma Kuzindua Mradi wa Maji ,Baada ya Kubaini Hitilafu

0

 

Mwenge ulivyopokelewa Kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu

KIONGOZI wa Mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2022 Sahili Geraruma, amegoma kuzindua mradi wa maji ulioko katika Kijiji cha Mwanduitinje Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, ambao umetekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilayani humo.

 

Mradi huo ambao ulikuwa uzinduliwe na Mwenge wa Uhuru leo, ulilenga kutoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 5823 wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakiangaika na huduma hiyo kwa muda mrefu.

 

Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge, amesema kuwa mradi huo utazinduliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Fauzia Hamidu mara baada ya kasoro nyingi ambazo mwenge umebaini zitakapofanyiwa kazi na wahusika.

 

Amesema kuwa wamebaini watendaji wamedanganya Mwenge kwa kutoa taarifa mabazo siyo sahihi kwao, mfumo wa uratibu hauko vizuri pamoja na maelezo ya watendaji ambao waliyatoa kutokueleweka.

 

“ Katika ukaguzi ambao tumefanya, mradi ni mzuri, umeanza kutoa maji kwa wananchi, kazi nzuri, ongera sana wale mliopewa dhamana ya usimamizi wa mradi kwani unaonekana, lakini jambo la kwanza tumebaini watendaji wamekuwa waongo ongo kidogo.” Amesema Geraruma.

Mradi wa Maji Uliotakiwa kuzinduliwa Kupitia Mbio za Mwenge, Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu

“ Sijui kwa nini wananidanganya Kiongozi, yaani kama wananidanganya mimi basi wanawadanganya wengine kuanzia Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na wengine wanaofuatia, lakini pia hata maelezo yao hayaeleweki na mfumo wa uratibu hauko vizuri,” ameeleza Geraruma.

 

Ameeleza kuwa kasoro nyingine ni ujenzi wenyewe wa mradi ambao baadhi ya sehemu hazijajengwa ipasavyo ikiwemo upakaji wa laki ambao siyo sahihi, chanzo cha maji kutokujengwa ipasavyo ikiwemo kuwepo mabomba yaliyopasuka na kuvuja.

 

“ Kwa kuwepo kwa kasoro hizo ambazo zinaonyesha mradi bado upo katika ujenzi mwenge wa uhuru unaagiza kasoro zote zilizobainika zifanyiwe kazi na mara baada ya kufanyiwa kazi na mradi kuwa vizuri Mkuu wa Wilaya atakuja kuzindua ili wananchi watumie maji,” ameeleza Geraruma.

 

Leave A Reply