The House of Favourite Newspapers

Uzinduzi wa Sinza Kwa Wajanja Marathon watikisa Dar

0

*Kusaidia wodi ya wazazi ya Hospitali ya Palestina

Uzinduzi wa mbio za Sinza Kwa Wajanja Marathon umefanyika jijini Dar es Salaam jana katika hafla iliyopambwa na shamrashamra mbalimbali huku mgeni rasmi akiwa ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge.

Sinza Kwa Wajanja Marathon inatarajiwa kufanyika Juni 16 mwaka huu katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, wilayani Kinondoni huku  wanariadha wakichuana katika mbio zenye umbali wa kilomita tano, 10 na 21 (nusu marathon), kulingana na mwenyekiti wa Klabu ya Marafiki wa Sinza, Bwana Geofrey Mhando.

Bwana Mhando alisema kwamba usajili wa Sinza Kwa Wajanja Marathon tayari umeshaanza na aliwasihi wadau wa michezo kujisajili ili kushiriki katika tukio hili la kihistoria.

Alisisitiza kwamba mbali ya kukuza maendeleo ya michezo, tukio hilo linalenga kukusanya fedha kusaidia wodi ya uzazi ya Hospitali ya Palestina.

“Tumejitolea kukuza afya njema nchini, ndio maana tumefanya uamuzi wa kuandaa tukio hili, sehemu ya fedha zitakazopatikana zitatumiwa kununua vifaa tiba kwa ajili ya wodi ya uzazi ya hospitali ya Palestina.

Tunatambua umuhimu wa Hospitali ya Palestina ya Sinza katika Wilaya ya Kinondoni, ikiwa msaada mkubwa si tu kwa wakazi wa Sinza bali pia kwa maeneo jirani, ni muhimu kuisaidia,” alisema Bwana Mhando.

Aidha alisema mbio hizo zitashirikisha wanariadha wote wa kitaifa na wengineo kwani lengo kubwa hasa si kupata washindi bali ni kusaidia maendeleo ya watanzania wenzetu hususan wanawake na watoto wanaopata huduma za afya katika Hospitali ya Palestina.

 

“Mbio hizi zinatumika si tu kuunganisha wakazi wa Sinza kutoka maeneo tofauti bali pia kurahisisha kubadilishana mawazo, hivyo, wakazi wa zamani wa Sinza na wengine kutoka ndani na nje ya Sinza wanakaribishwa,” aliongeza.

 

Bwana Mhando pia aliongeza kuwa kabla ya mbio kuanza, tarehe 15 Juni, kutakuwa na hafla ambayo wajasiriamali wataonyesha bidhaa zao kwenye viwanja vya Posta, ikiambatana na shamrashamra mbalimbali za burudani.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, alipongeza waandaaji wa Sinza kwa Wajanja Marathon kwa tukio hilo litakalochangia kuhamasisha maendeleo ya michezo na afya njema kwa wakazi wa Sinza na maeneo jirani huku akihamasisha wadau wa michezo nchini kushirikiana na waandaaji kufikia malengo yao.

 

“Hii ni wazo zuri sana, hasa kwa Sinza Kwa Wajanja Marathon, ambayo inafanyika mara ya kwanza, nawasihi wadau wote kusaidia waandaaji na kushiriki kwenye tukio huli,” alisema Mstahiki Meya akizindua rasmi tukio hilo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Bwana Dama Lusangija, alisema kwamba mbio hizo zitaongeza hamasa kwa wakazi wa maeneo hayo na maeneo jirani ili kujenga tabia ya kufanya mazoezi na kudumisha afya njema.

 

“Tunashukuru waandaaji kwa kuandaa mbio hizi, zinazofanyika kwa mara ya kwanza kwa wakazi wa Sinza na maeneo jirani, hili ni tukio la kihistoria ambalo litakuza si tu afya njema bali pia kukuza maendeleo ya michezo,” alisema Bwana Lusangija.

 

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mabatini, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ASP) Soty Mtaki alisema kuwa wamejiandaa kutoa usalama kwa washiriki wote kabla na wakati wa mashindano.

Baadhi ya wadhamini wa Sinza Kwa Wajanja Marathon ni, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo, Kampuni ya ulinzi ya SGA, IceDrop, Switch, Kuambiana Investment, Azam Media, Mapembelo Cargo na Gentlemen Club.

Leave A Reply