KISA FEDHA ZA RAISI JPM… BIBI YAMFIKA MAZITO!

IKIWA unaishi maisha yako kwa raha mustarehe, afya yako ikiwa njema, unapaswa kushukuru kwani upande wa pili kuna wengine wanataabika na maradhi mbalimbali huku wakiwa hawana uwezo wa kupata matibabu. 

 

Gazeti la Kufichua Maovu, Uwazi lina habari ya Happifania Tindwa (75), mkazi wa Mtoni Kwa Azizi Ali, jijini Dar ambaye amefikwa na mazito yaliyosababisha auguze majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake, akiwa hana msaada wowote.

 

Akizungumza kwa tabu, juzi jijini Dar es Salaam, Happifania alidai kuwa, chanzo cha mateso hayo ni kipigo alichopewa na mjukuu wake aliyemtaja kwa jina la Fimbo Machupa. “Nakufa nikijiona, fedha za Tasaf nilizopewa msaada zinageuka maumivu kwangu. Namshukuru sana Rais (Dk. John Magufuli) wangu kwa kutukumbuka sisi masikini, lakini pesa hizo zinataka kunitoa roho,” alisema bibi huyo kwa uchungu.

 

ILIKUWAJE?

Akisimulia kisa kizima, bibi huyo alisema chanzo cha matatizo yaliyomwingiza kwenye dira mpya ya maisha yake ni kwenda kuishi kwa dada yake, Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani ambapo akiwa huko aliunganishwa katika mfuko wa kusaidia wazee na wasiojiweza wa Tasaf.

 

“Nilipokuwa kwa dada yangu, akaniambia kuna mfuko wa kusaidia wazee na watu wasiojiweza, nikasaidiwa kuunganishwa. Nikawa napata Shilingi 50,000 kila baada ya miezi mitatu. “Kwa sababu ya uzee wakati mwingine fedha zangu na za dada zikawa zinafuatwa na mtoto wa dada yangu anayeitwa Machupa. Mwanzo akawa ananipa fedha zangu vizuri tu, lakini kuna muda ukapita, nikashangaa sipatiwi fedha, nikiuliza naambiwa fedha hazijatoka.

 

“Kuna siku nikaamua kumuuliza mzee mwenzangu mwingine ambaye naye yupo katika mpango huo, akaniambia fedha zinatoka kama kawaida. Hata ile miezi ambayo niliambiwa fedha hazijatoka, nikaambiwa zimeshatoka,” alisimulia bibi huyo na kuongeza: “Nilipoambiwa pesa zangu amechukua Machupa nikamfuata na kumwuliza kwa nini amechukua pesa zangu muda mrefu na hanipi, anakaa kimya tu akawa hanipi majibu ya kueleweka.”

TATIZO LIPO HAPA

“Ukweli alivyonijibu vile, nilipata hasira na kwa kuwa ni mtoto wa dada yangu, ni mwanangu pia, nilimvaa nikitaka kumtandika lakini tukiwa kwenye purukushani alitokea mwanaye aitwaye Fimbo akaingilia na kunipiga na gongo kama kuni sehemu mbalimbali za mwili wangu, hicho ndiyo chanzo cha haya madonda mnayoyaona,” alisema bibi huyo akiwaonyesha waandishi wetu majeraha makubwa aliyonayo, akiwa ameumia zaidi sehemu ya kalio moja.

 

Anasema baada ya kitendo hicho, walimbeba na kumrudisha Kwa Azizi Ali, nyumbani kwa watoto wake ambapo alikuwa akiishi kabla na wanaye hao.

 

FIMBO ABANWA, AFUNGUKA

Katika kuweka usawa wa kihabari, Uwazi lilimsaka mjukuu wa bibi huyo, aitwaye Fimbo Machupa anayedaiwa kumpiga bibi huyo na kumsababishia majereha ambapo alifunguka: “Huyo bibi mimi sijawahi kumpiga hata kidogo, hayo mambo yao ya kudhulumiana pesa mimi hayanihusu hata kidogo, nayasikia tu.”

 

Alikiri bibi huyo kwenda kwao Bagamoyo kuwatembelea, lakini suala la kumpiga alipinga akisisitiza: “Yule bibi kutokana na uzee, huwa ana matatizo ya kuanguka, sasa kuna siku alianguka kwenye moto na kupata hayo majeraha. Mimi siwezi kumpiga bi kizee kama huyo.” Fimbo alizidi kugongelea msumari: “Hata hivyo mimi ndiye niliyemrudisha huko Dar kwa watoto wake, sasa kama nina ugomvi naye, ningemrudisha vipi mpaka kwa hao watoto wake?”

 

MARADHI YA BIBI

Katika kuzidi kufuatilia habari hiyo, wanahabari wetu walizungumza na mtoto wa bibi huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Paschal Mhagama ambaye alieleza taarifa ya hospitali na namna anavyofahamu kisa cha mama yake kupata maswahibu hayo.

 

“Ndugu zangu, mama yangu aliondoka hapa kwenda kuishi na dada yake huko Mapinga (Bagamoyo) akiwa salama kabisa, lakini nikashangaa wiki iliyopita kaka yangu binamu aitwaye Machupa alimrudisha na kusema anaumwa naye hakuwa na muda wa kukaa kutueleza vizuri aliondoka muda huohuo.

 

“Nilipomwangalia mama yangu nikagundua yuko katika hali mbaya na hawezi hata kuzungumza, nikamkimbiza hospitalini (Temeke) ambapo alipatiwa matibabu mpaka alipopata nafuu. Akiwa hospitali ndipo alionekana kuwa na madonda makubwa mwilini.

 

“Alikuwa hajiwezi, hakuwa hata anaweza kujieleza mwenyewe. Alipopata fahamu na kuhojiwa ndiyo akamtaja kijana Fimbo kuwa ndiye alimfanyia ukatili huo kwa kumpiga na gongo alipokuwa akidai pesa zake za Tasaf,” alisema.

 

Uwazi lilipompa maelezo ya Fimbo kukanusha madai hayo, akidai ndiye aliyempeleka nyumbani hapo, alisema: “Ni muongo mkubwa, aliyemleta mama hapa nyumbani ni baba yake (Machupa). Yeye hajakanyaga hapa.”

 

Kuhusu matibabu, Mhagama alisema wamepata matibabu ya awali lakini wanashindwa kuendelea na tiba ya uhakika kwa sababu hawana fedha. “Kama mnavyoona ndugu waandishi, tunaishi maisha duni hapa nyumbani. Mama anatakiwa tiba zaidi ili kumsaidia kupona, hali yake ni mbaya sana, tunaomba sana wasamaria wema watusaidie,” alisema Mhagama.

 

KUTOA NI MOYO

Ndugu msomaji, bibi huyo yupo katika mateso makali ya maradhi. Anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kutibiwa. Msaada unaweza kuwa wa fedha, matibabu au sheria ili kumsaidia bibi huyo kupata haki yake. Kwa yeyote aliyeguswa, wasiliana na mhariri kwa namba 0658-798787 utaunganishwa naye.

STORI: ZAINA MALOGO NA RICHARD BUKOS, DAR

 

Loading...

Toa comment