KISHINDO NDOA YA BABU SEYA!

DAR ES SALAAM: “Jamani Babu Seya huyuhuyu aliyefungwa kifungo cha maisha gerezani ndiye anaoa?”  “Ndiye huyohuyo ambaye jina lake kamili ni Nguza Viking; Septemba 7, mwaka huu anafunga ndoa ambayo itakuwa na kishindo kikuu.”

 

Hayo yanaweza kuwa mazungumzo ya kihisia wakati unasoma habari hii ambayo Gazeti la Ijumaa linakupakulia baada ya kunasa mchongo kuwa mzee baba yupo mbioni kuvuta jiko. Uzembe kwetu mwiko, hivyo mbali na kuwepo kwa habari hiyo, mwandishi wetu alifanikiwa kufanya mahojiano maalum (exclusive) na Babu Seya baada ya kumfungia safari hadi nyumbani kwake, Mbezi-Beach jijini Dar na kutoa mchongo nzima.

KISHINDO KIKOJE?

Mwandishi wetu alipofika eneo analoishi mzee huyo, kwanza alipitapita kwa baadhi ya majirani na kubaini kuwa ndoa hiyo itakuwa ya aina yake kutokana na watu wengi kuichukulia kama muujiza.

 

“Mimi nimeletewa kadi ya mwaliko, kusema kweli nilishtuka, lakini baadaye nikamshukuru Mungu hadi machozi yakawa yananitoka. “Mtu (Babu Seya) aliyekuwa amefungwa maisha na kuonekana kama anafia gerezani, leo ametoka na anaoa; kwangu hili ni jambo la kipekee,” alisema mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Baba Francy.

 

MAANDALIZI YAKE NI MOTO

Chanzo kililiambia Gazeti la Ijumaa kuwa, sehemu kubwa ya maandalizi ya sherehe hiyo yamekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni siku ya tukio. “Itakuwa sherehe ya kukata na shoka, itakuwa ya kula na kunywa hadi kusaza, burudani za kila aina zitakuwepo.

“Nafikiri unajua kuwa Nguza ni mwanamuziki, mtoto wake Papii Kocha (Johnson Nguza) naye ni mwanamuziki tena wa kizazi kipya, kwa hiyo burudani zitakuwa si za kawaida. “Wasanii wasiokuwa na idadi wa kila rika watakuwepo, yote hiyo ni kuifanya siku hiyo kuwa ya kipekee.

“Tumealika watu wengi wakiwemo viongozi wa Serikali na tunaamini kuwa watafika kuja kumuunga mkono mzee wetu ambaye kimsingi ni kipenzi cha watu,” chanzo kilimaliza kusema.

HODI KWA BABU SEYA

Kufanya mambo yasiwe mengi, mwandishi wetu alimfuata muoaji mwenyewe ili kujua kwa undani kile kinachosemwa kuhusu ndoa yake ya kishindo anayotarajia kufunga.

Mambo ya msingi ambayo pengine ungependa kujua ni; vipi Babu Seya alikutana na huyo mkewe mtarajiwa? Ni nani hapa mjini, watoto wake wamepokeaje uamuzi wake wa kuoa na kwa nini mzee huyo ameamua hivyo wakati umri umesogea? Usijali yote muoaji ameulizwa na kuyapatia majibu.

BABU SEYA:

Huyu mwanamke ninayetaka kumuoa nilikutana naye baada ya kutoka jela mwaka 2017.

MWANDISHI: Basi mimi nilifikiri kuwa ulikuwa naye kabla na kwamba ulipotoka ukakumbuka hame lako?

BABU SEYA: Hapana, ni baada ya kutoka! Mapenzi yalipokolea kwake ndiyo nikafikia uamuzi huu wa kuoa.

MWANDISHI: Unaoa huku ukiwa na watoto wakubwa, ulipowaambia juu ya uamuzi huu walikuruhusu?

BABU SEYA: Kabisa…kabisa, kwanza bila wao kuniruhusu nisingefanya hivi; kwa hiyo wako radhi kupata mama mpya.

MWANDISHI: Hili linaweza kuwa swali la uchokozi kidogo; inaonekana umri wako ni mkubwa, kwa nini usingeacha kuoa maana kuoa kunahitaji nguvu wakati mwingine.

BABU SEYA: Hahahaha (anacheka kidogo) mimi nahitaji mtu wa kunilinda usiku, kwa hiyo lazima nioe bwana.

MWANDISHI: Mashabiki, marafiki wangependa kumjua huyo mkeo mtarajiwa pengine kwa jina au hata kumuona kwa picha.

BABU SEYA: Anacheka sana kisha anaendelea: Ungesahau kuuliza hilo ningeshangaa; mke wangu watamuona siku hiyo ya harusi na picha yake sikupi, ukitaka kumuona usikose kwenye shughuli yenyewe.

MWANDISHI: Hebu nipe utamutamu wa shughuli yenyewe utakavyokuwa.

BABU SEYA: Mimi ni mtu wa watu, shughuli itafana sana, itakuwa ya kipekee. Kikubwa kwa sababu Global (Publishers) ni ndugu zangu, msikose siku hiyo.

BABU SEYA NI NANI?

Ni mwanamuziki maarufu nchini mwenye asili ya nchi ya DR Congo ambaye Juni 5, 2004, alijikuta matatani kwa kuhumiwa kifungo cha maisha yeye na mwanaye Johnson Nguza (Papi Kocha), baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa makosa ya unajisi watoto.

Baada ya harakati nyingi za kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, Babu Seya na mwanaye hatimaye waliachiwa huru Septemba 10, 2017 kwa msamaha wa Rais Dk John Pombe Magufuli, baada ya kutumikia adhabu yao kwa kipindi cha miaka 13.

Babu Seya alifiwa na mkewe kabla ya kuhukumiwa na kwamba tangu ametoka jela amekuwa akiishi maisha ya upweke ambapo mara kadhaa alisikika akisema amekuwa hapendi kuishi hivyo.

Aidha, mwanamuziki huyo baada ya kutoka na kuanza maisha mapya uraiani, amekuwa akijihusisha na shughuli za muziki kujaribu kujenga upya maisha yake, ambayo yaliharibika alipopata matatizo.


Loading...

Toa comment