The House of Favourite Newspapers

Shigongo: Ndege Yetu Kuzuiliwa Afrika Kusini, Uzalendo Wetu Unajaribiwa!

DIARY ya Shigongo:

NI Jumamosi nyingine, naendelea na shughuli zangu za ujenzi wa taifa na nikiwa natafakari mambo mbalimbali yanayoendelea nchini, nakutana na taarifa ya msemaji wa serikali, ndugu yangu na rafiki yangu, Dk. Hassan Abbas.

 

Akiwa jijini Dodoma, Dk. Abbas anasikika akisema Watanzania wote ambao kwa namna moja au nyingine watabainika kuihujumu serikali katika sakata la kuzuiwa kwa ndege ya serikali nchini Afrika Kusini, watafunguliwa mashtaka mahakamani kwa kosa la kuihujumu nchi.

 

Ndugu zangu, tangu kuibuka kwa sakata la kuzuiwa kwa ndege yetu, Airbus A220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng jijini Johannesburg, Afrika Kusini, tumeshuhudia mengi ya kusikitisha na kutia aibu.

 

Mara tu baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Leonard Chamburiho, Agosti 23, mwaka huu kutangaza kwamba ndege yetu imezuiliwa nchini Afrika Kusini, kuliibuka mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

 

Baadhi ya Watanzania wenzetu, bila kuwa na hata chembe ya aibu, walianza kujitokeza na kushangilia kukamatwa kwa ndege yetu. Kwao, hizo zilikuwa ni taarifa njema sana, wameendelea kutamba kwenye mitandao ya kijamii kwa siku zote hizo, kila siku wakiibuka na ‘vibonzo’ vipya vya kushangilia suala hilo.

 

Hawa wanaoshangilia, siyo kwamba ni raia wa Burundi au Kenya, ni Watanzania wenzetu. Unaweza kutathmini sisi kama taifa tumefikia kwenye hali mbaya kiasi gani. Uzalendo wetu unapitia kwenye kipimo kikubwa.

 

Jitihada kubwa za kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zimefanywa na serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli. Kama utakuwa umesahau, ngoja nikukumbushe jambo.

 

Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakipigiwa sana kelele na wapinzani kabla Rais Magufuli hajaingia madarakani, ilikuwa ni nchi kukosa ndege yake na badala yake, kutumia ndege ya kukodi, tena chakavu. Wanasiasa wa upinzani walipiga sana kelele kwenye majukwaa ya siasa na kiukweli lilikuwa ni jambo ambalo lilitusononesha wengi.

 

Kwa nini nchi ambayo imejaaliwa rasilimali za kila aina, miaka hamsini baada ya uhuru wake inashindwa hata kumiliki ndege yake moja? Rais Magufuli alipoingia madarakani, aliamua kulivalia njuga suala hilo na matokeo yake wote tunayaona. Ndani ya muda mfupi tu, ndege zilianza kuwasili nchini.

 

Ziliwasili Bombadier Q400 Dash 8 mbili, ikaja Bombadier CS300 na Boeing 787-8 Dreamliner, zikatua Airbus A220-300 mbili, moja ikipewa na jina la Ngorongoro na nyingine ikipewa jina la Dodoma.

 

Kama hiyo haitoshi, Rais Magufuli akaagiza ndege mbili za rais, kati ya tatu, Fokker 28 na Fokker 50, nazo zianze kutumiwa na ATCL kwa ajili ya kusafirisha abiria. ATCL ikawa imefufuka rasmi, ndege zetu zenye nembo ya twiga mkiani zikawa zinaonekana kwenye viwanja vikubwa vya ndege, angalau sasa ile aibu iliyotutafuna kwa zaidi ya miaka hamsini, ikawa imeisha.

 

Najua Watanzania wengi siyo watumiaji wakubwa wa usafiri wa ndege, lakini kwa wale wachache ambao huwa wanatumia usafiri huo, iwe ni kwa safari za ndani au safari za nje, watakuwa wanajua ni fahari ya kiasi gani ambayo mtu huipata anaposafiri kwa ndege zetu, zilizonunuliwa kwa kodi zetu, kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

 

Sasa unashindwa kuelewa, hawa wenzetu wanaofurahia ndege yetu kukamatwa, wao wapo katika kundi gani? Wanachokishangilia ni nini? Ina maana haya mafanikio makubwa yaliyofikiwa na serikali hii, wao hayawahusu? Ni jambo la kusikitisha sana.

 

Ukifuatilia kwa makini sakata zima la kukamatwa kwa ndege yetu, lina historia ndefu ambayo haijaanza jana wala juzi. Mzungu Hermanus Steyn ambaye amewahi kuishi nchini na kumiliki vitega uchumi kadhaa kabla ya baadaye kutaifishwa na kuamriwa kuondoka nchini, ndiye anayetusumbua!

 

Ndiye aliyesababisha ndege yetu ikamatwe. Siyasemi haya kwa lengo la kujenga chuki dhidi ya Mzungu huyu, hapana! Pengine na yeye anatapatapa akiwa anatafuta nafasi ya kurejesha mali zake. Mali zake zilitaifishwa Januari 17, 1982 na kuna historia ndefu kidogo kwenye sakata hili.

 

Kipindi hicho rais hakuwa Magufuli, ni zama za hayati baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hiyo inathibitisha kwamba hiki kinachoendelea, ni vita ya kiuchumi ambayo inalihusu taifa zima na siyo chama wala mtu mmoja.

 

Inapotokea familia ikawa inashambuliwa na maadui, tunafundishwa kwamba hata kama ndani baba na mama hawakuwa na maelewano mazuri, au watoto walikuwa na mikwaruzano yao ya hapa na pale, wote wanatakiwa kuweka tofauti zao pembeni kwanza na kupambana kama familia dhidi ya adui.

 

Matatizo yakiisha, ndipo wanapoweza kurudi kwenye meza ya majadiliano na kila mmoja akaeleza dukuduku lake. Ni jambo la ajabu sana kwamba familia inakuwa na ugomvi na maadui kutoka nje, halafu mtoto anatoa siri kwa maadui ili waweze kuiteketeza familia hiyo.

 

Hiki ndicho kinachotokea kwa sasa, kama taifa tunapitia kipindi kigumu, ndege yetu imeshikiliwa nchini Afrika Kusini, kama familia moja ya mama Tanzania, tunatakiwa kushikamana na kuwa kitu kimoja kupambana kuhakikisha ndege yetu ambayo imenunuliwa kwa kodi za kila Mtanzania, inarudishwa salama nchini.

 

Lakini hapohapo wanaibuka watu na kushangilia, wanatamba mitandaoni wakiwa wamejificha nyuma ya ‘keyboard’ za kompyuta zao au nyuma ya simu zao za kisasa (smartphones). Wanajifanya Tanzania haiwahusu, wanaomba mabaya yaendelee kuikumba nchi yetu kwa sababu tu pengine kuna mtu haipendi CCM au hampendi Rais Magufuli kwa sababu zake binafsi.

 

Wanachoshindwa kuelewa ni kwamba haya mambo ya vyama ni mambo ya kupita tu, CCM leo ipo kesho haitakuwepo. Chadema leo ipo kesho haitakuwepo lakini Tanzania itaendelea kuwepo. Hata mimi na wewe tusipokuwepo, bado vizazi vyetu vitaendelea kuwepo kwa sababu Tanzania ndiyo sehemu ambayo Mungu amewapangia kuishi.

 

Maana yake ni kwamba Utanzania ni kitu kikubwa na cha thamani kuliko haya mambo ya itikadi za vyama au tofauti zetu za kisiasa.

Naunga mkono kile alichokisema Dk. Abbas, kama kweli kuna watu watakuja kubainika kwamba ndiyo waliokuwa wakishirikiana na maadui zetu kutudhoofisha, wachukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha mambo ya aina hii.

 

Uko wapi ule uzalendo wetu? Tukiwa shule za msingi tukikimbia mchakamchaka, tulikuwa tukiimba nyimbo za kizalendo na kufundishwa kuipenda nchi yetu. Uzalendo ule uko wapi? Kama taifa, kuna mahali tumejikwaa na tunapaswa kurekebisha tofauti zetu haraka iwezekanavyo.

 

Binafsi nawatakia kila la heri wanasheria wetu waliosafiri kwenda nchini Afrika Kusini kufuatilia ndege yetu, najua jitihada kubwa zinafanywa na watu wenye uzalendo wa kweli kwenye mioyo yao kuhakikisha Tanzania yetu inakuwa salama.

 

Watanzania wote wenye uzalendo wa kweli ndani ya mioyo yetu, tuendelee kushikamana. Tusikatishwe tamaa na hawa wenzetu wachache wanaoiombea mabaya nchi yetu.

Naamini busara kubwa itatumika kumaliza huu mvutano kati ya serikali na bwana Steyn na hatimaye mambo yatarudi kwenye mstari.

Mungu ibariki Tanzania.

Ahsanteni kwa kunisoma.

Ndege ya ATCL iliyozuiliwa Afrika Kusini

Comments are closed.