The House of Favourite Newspapers

Kisutu: Wema Atinga Kortini na Wakili Mpya

Wema Sepetu akiwa mahakamani.

KESI  ya mrembo Wema Sepetu ya kukutwa na msokoto wa bangi imesikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Inspekta wa Polisi, Wille ameieleza mahakama kuwa hakuwepo wakati mtuhumiwa huyo  akichukiliwa sampuli ya mkojo kwa Mkemia Mkuu wa serikali.

Shahidi huyo ameyaeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati alipoulizwa maswali na Wakili wa Wema Sepetu, Alberto Msando.

 

Katika ushahidi wake, Inspekta Wille, alidai hakuwahi kupeleka sampuli za mkojo  za washtakiwa wenzake wa Wema ambao ni Angelina Msigwa na Matrida Abbas kwenda kuchunguzwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Inspekta Wille alidai kuwa February 8, 2017 alifika katika ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali saa 5 asubuhi na kumkabidhi Mchunguzi Elia Mulima kichupa cha plastiki ambacho ndani kilikuwa na mkojo wa Wema.

 

 

Wakili Msando alimuuliza Inspekta Wille kama alikuwepo wakati sampuli ya mkojo uliokuwamo ndani ya kichupa cha plastiki unachukuliwa ambapo  alijibu kuwa hakuwapo kwa wakati huo.

Msando alimuhoji Inspekta Wille kuwa walikaa kwa muda gani katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo Inpekta Wille alidai kuwa hakumbuki.

Katika maelezo yake, pia Inspekta Wille alidai yeye hakupekuwa katika chumba anacholala Wema bali alipekuwa katika chumba anachohifadhia nguo na viatu.

Aliendelea kuiambia mahakama kwamba katika upekuzi wao walikuta msokoto wa bangi jikoni juu ya kabati, pia walikuta msokoto wa bangi uliotumika ukiwa ndani ya kiberiti dirishani katika chumba wanacholala wafanyakazi  wawili wa Wema.

Baada ya kueleza hayo, aliiomba mahakama ipokee hati ya ukamataji mali iliyojazwa katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo  kama kielelezo ambapo mahakama ilipokea.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 26 na 27, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

 

NA DENIS MTIMA/GPL

Comments are closed.