The House of Favourite Newspapers

KITIMTIM DAWA NGUVU ZA KIUME

NI kitimtim dawa za nguvu za kiume! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali kupitia kikosi kazi cha Manispaa ya Ilala jijini Dar kuvamia bohari ambayo awali ilidaiwa ilikuwa na shehena ya dawa za kuongeza nguvu za kiume zilizopitisha muda wake.  

 

Hata hivyo, baada ya kikosi hicho kuvamia bohari hiyo hivi karibuni, ilibainika dawa hizo zinakwisha muda wake mwishoni mwa mwezi huu.

TUJIUNGE NA CHANZO

Chanzo cha habari hizi kililitonya Ijumaa Wikienda kuwa pamoja na mambo mengine, kikosi kazi hicho cha watumishi wa Serikali kimepanga kuibuka katika bohari hiyo kwa kushtukiza kufuatia kuwepo kwa madhara makubwa yanayotokana na watumiaji wa madawa hayo.

Chanzo hicho kilisema, baadhi ya watumiaji wa dawa hizo wamekuwa wakifia kwenye nyumba za wageni baada ya kuzidisha dozi wanapohisi hazifanyi kazi vizuri. “Unajua mtumiaji anaweza kutumia kama anavyoelekezwa lakini pengine vidonge vimeisha muda wake hivyo havimpi nguvu anayotaka hivyo wengi wanaamua kujiongezea dozi ili wafikie lengo, lakini kumbe wanakuwa wakijisababishia madhara na pengine kifo,” kilisema chanzo hicho.

KIKOSI KAZI MZIGONI

Kikosi kazi hicho kikiongozwa na mfamasia kutoka Manispaa ya Ilala, Aidan Ally na maofisa afya wa manispaa hiyo, kiliingia kwa kushtukiza kwenye bohari hiyo iliyopo maeneo ya Vingunguti, Barabara ya Nyerere jijini Dar na kuzua kitimtim kutokana na ugeni huo wa ghafla.

UPEKUZI MZITO

Mara baada ya kufika kwenye bohari hiyo, maofisa hao walifanya upekuzi wao na kukuta shehena za madawa mbalimbali ikiwemo dawa za nguvu za kiume aina ya Kamagra ambazo muda wake wa kutumika ulionesha kumalizika mwishoni mwa mwezi huu tofauti na taarifa za uchunguzi wa awali zilizodai muda wake ulishamalizika.

Baada ya wakaguzi hao kujiridhisha kuwa bohari hiyo haikuwa na makosa walimwambia mmiliki wake kuwa ahakikishe dawa hizo zinazomalizika muda wake mwishoni mwa mwezi huu aziuze haraka kabla ya kupitisha muda wake vinginevyo ataingia hatiani.

MFANYABIASHARA AJIBU

Mfanyabiashara huyo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja aliitikia wito huo na kusema kamwe hawezi kuuza dawa iliyokwisha muda wake kwani hata hizo dawa ambazo zinamaliza muda wake mwezi huu kama zisiponunuliwa atafanya taratibu za kuziteketeza kwa kuzihusisha taasisi husika.

NGUVU ZA KIUME NI TATIZO

Hivi karibuni tatizo la nguvu za kiume limeonekana kuwa kubwa kwa wanaume wengi hali iliyoongeza watumiaji dawa za vidonge na za mitishamba ambapo wengine zimekuwa zikiwadhuru na kuwasababishia umauti.

CHANZO CHAKE

Madaktari mbalimbali wameeleza kuwa, chanzo kikubwa cha tatizo hilo ni aina ya vyakula tunavyokula vyenye mafuta, kutofanya mazoezi na pia msongo wa mawazo.

MTAANI MABANGO

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo husasan kwa miaka ya hivi karibuni, watu wengi wamekuwa wakitumia changamoto hiyo kama fursa ya kujiingizia kipato kwa kusema wanatibu tatizo hilo kwa mitishamba. Hata hivyo, wengi wao wamedaiwa kufanya hivyo kwa ajili ya kuwalaghai tu watu na dawa hizo hazitibu.

TAMKO LA SERIKALI

Kutokana na wimbi hilo la waganga wanaodai kutibu, Julai 2016, Serikali ilitoa tamko na kuzitaja dawa ambazo zinaruhisiwa kutumika kwa ajili ya kuongeza nguvu za kiume kwa kuzingatia ushauri wa daktari.

AFISA UHUSIANO TFDA ALISEMA

Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza, alisema ni kweli kuna dawa nyingi zinazotangazwa na watu mbalimbali kuwa zinatibu tatizo la nguvu za kiume, lakini zilizo rasmi ni pamoja na Viagra, Erecto, Cialis na Suagra.

Simwanza alisema dawa hizo ndizo wanazozitambua kuwa zinaweza kutumiwa na watu waliopungukiwa au kuishiwa kabisa nguvu za kiume kwa sababu zimepitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kitaalam. Hata hivyo, Simwanza alisema dawa hizo siyo za kutumiwa kiholela bali wenye shida nazo ni lazima wafuate maelekezo ya madaktari ili kujiepusha na madhara yake pindi zikitumika kiholela.

“Kuna dawa nyingi ambazo sisi tunazitambua na tumezipitisha zitumike…lakini mtu asizitumie hadi pale atakapopewa ushauri wa daktari. Hizi zina nguvu sana na zinaweza kufanya mishipa ya moyo kupasuka au kuathiri mfumo wa damu kwa watu wanaozitumia bila kufuata maelekezo ya madaktari,” alisema Simwanza.

STORI: Richard Bukos, DAR

Comments are closed.