The House of Favourite Newspapers

Kocha Yanga Awatoa Hofu Mashabiki, Zesco Tunawafunga – Video

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera.

KOCHA wa Yanga Mwinyi Zahera amewasisitiza mashabiki wa timu hiyo kutembea kifua mbele wala wasitishwe na sare ya jana ya bao 1-1 dhidi ya Zesco kwenye Uwanja wa Taifa.

 

Yanga ililazimishwa sare hiyo kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku timu hizo zikirudiana Septemba 27 ugenini mjini Ndola. Bao la Yanga lilifungwa na Patrick Sibomana dakika ya 25 kwa mkwaju wa penati huku lile la Zesco likipachikwa na Thabaan Kamusoko kwa shuti kali la nje kidogo ya 18 dakika ya 90+4.

Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili isonge mbele kwenye hatua ya makundi. Lakini ikishindwa kupata matokeo kwenye mchezo huo itaangukia katika hatua ya mtoano katika Kombe la Shirikisho kuwania kuingia kwenye makundi.

 

Licha ya mashabiki wa Yanga kuonekana kunyongea kutokana na bao la usiku pamoja na kejeli za wenzao wa Simba ambao walikuwa wakiishangilia Zesco ya George Lwandamina, Zahera amewatoa hofu. Zahera amesisitiza kwamba; “Kutoka na sare hii haimaanishi kwamba tumetoka, kwa vile tuna uwezo wa kwenda kushinda bao 1 ugenini kama tulivyofanya kwa Township Rollers.”

“Kwanza leo(jana) nitalala usingizi kwa vile timu yangu imecheza vizuri na wachezaji wamefuata maelekezo yangu, walikosa bahati tu kwani walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuweza kuingiza goli,”alisisitiza.

 

“Hata kama tungeshinda kwa lile bao moja lazima kule tungelazimika kwenda kushinda bao lingine ili tuwe na uhakika wa kupita, kwa hiyo sare hii haijabadilisha chochote sababu bado mchezo unaendelea,”aliongeza Zahera kwa kujiamini.

Lwandamina kwa upande wake alisema; “Yanga ni timu nzuri nimeiona, inacheza kuanzia nyuma mpaka mbele na ilitupa wakati mgumu kutengeneza nafasi na tulishindwa kucheza mchezo wetu.”

Kamusoko ambaye aliondoka Yanga hivi karibuni alisema; “Siwezi kuizungumzia Yanga lakini nafurahia rekodi yetu ya kutopoteza mchezo pale nyumbani kwetu Ndola.” Lakini Zahera akadakia kwa kusisitiza kwamba; “Kamusoko hajaonyesha mchezo wowote ambao ulinifanya nijute
kumuacha. Lile goli tu ndio limembeba.”

VIPENSI Katika mchezo wa jana Zahera aliendelea kutinga kipensi chake huku mashabiki kibao wakimuunga mkono kwa kuvaa aina hiyo ya mavazi kuanzia uwanjani mpaka mitandaoni.

Zahera alisema kwamba anaamua kuvaa aina hiyo ya mavazi kutokana na hali ya hewa ya joto na kama kungekuwa na baridi angepigilia suti. Katika mchezo wa jana Yanga ilianza kwa kasi kwa kuhakakikisha wanapata bao la mapema huku ikitumia viungo wanne. Mshambuliaji wa kigeni wa Yanga, Sadney Urikhob ameendelea kuwa mwiba kama ilivyokuwa kwa Township Rollers baada ya kutengeneza penalti iliyozaa bao la kuongoza.

 

Zesco walifanya mashambulizi kadhaa lakini hayakuwa na madhara na hawakucheza soka lao lilizoweleka kutokana na kiwango cha Yanga. SIBOMANA Patrick Sibomana, mshambuliaji wa Yanga, Jana aliwaziba mdomo mashabiki wa Simba waliojitokeza kuipa sapoti timu ya Zesco kwenye mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.


Kabla ya Sibomana kupachika bao la penalti kipindi cha Kwanza, zomea zilikuwa nyingi kwa mashabiki hao ambao walitinga uwanjani na jezi za Zesco na waliamini kuwa penalti itakoswa na nyota huyo. Utulivu na umakini wa Sibomana ulimfanya apachike bao la penalti ambalo liliwakalisha chini na kuwanyamazisha mashabiki wa Simba Uwanja wa Taifa.

 

Mashabiki wa Yanga kama kawaida yao waliwazomea kimtindo watani zao kisha wakaendelea kuishangilia timu yao Uwanja wa Taifa. Yanga; Metacha, Sonso,Yondani,Feisal Salum,Mapinduzi Balama,Mohamed Juma, Sibomana,Urik hob,Makame,Tshishim bi, Lamine Moro.

STORI NA BRAHIM MUSSA NA LUNYAMADZO MLYUKA, DAR

Comments are closed.