Baharia Papii Kocha, mrembo live

JAPO inaaminika kuwa neno Baharia ni mtu anayefanya kazi kwenye chombo cha usafiri majini, hasa baharini kama vile boti, mashua, jahazi au meli lakini usemi huu umekuwa maarufu na kubadilishwa maana yake kwa kasi ambapo tafsiri isiyo rasmi inamaanisha mtu anayefanya mambo pasipokutarajia.

 

Msanii wa Muziki wa Dansi, Johnson Nguza ‘Baharia Papii Kocha’ amenaswa live na mrembo muda mfupi baada ya baba yake ambaye pia ni mkongwe wa muziki huo, Nguza Viking ‘Babu Seya’ kufunga ndoa.

 

TUJIUNGE

Wawili hao walianza kuonekana pamoja siku ambayo Babu Seya alikuwa akifunga ndoa na mkewe, Katibu Tawala Wilaya ya Muheza, Desderia Haule katika Kanisa Katoliki Sinza jijini Dar ambapo muda mwingi walionekana bize kama mtu na mpenzi wake.

Licha ya kuonekana hivyo, maneno yalikuwa mengi nje ya kanisa hilo huku kila mmoja akiongea yake.

“Naona wameamua sasa, baba amefunga ndoa na mtoto naye anajiandaa kufunga,” alisikika mmoja wa wahudhuriaji kanisani hapo mara baada ya kutoka nje.

 

UKUMBINI SASA

Paparazi wetu aliendelea kuungana nao hatua kwa hatua, jino kwa jino hadi katika Ukumbi wa Hotel ya Landmark, Mbezi Beach jijini Dar kulikofanyika sherehe hiyo ambapo ndani ya muda mfupi, mrembo huyo aliingia pamoja na Papii wakiwa wameshikana mikono na kwenda kukeketi siti moja.

 

MUZIKI WAWAKOLEA

Wakati taratibu nyingine zikiendelea ukumbini hapo, Papii na mrembo huyo aliyekuwa amevalia gauni jekundu hawakuonesha utulivu.

Walishikana mikono na kunyanyuana kisha kuanza kucheza muziki huku mrembo huyo akimshikilia kiuno Papii jambo lililowaibua wananzengo wengine waliopo ukumbini.

“Anajua kutendea haki muziki, ona walivyoshikana viuno hapa si bure Papii ameshachukua jiko tusubirie kualikwa ndoa yao baada ya hii ya baba yake,” alisikika mhudhuriaji mwingine ukumbini hapo.

 

MSIKIE PAPII

Kupata uhakika wa uhusiano huu ambao kwa mara ya kwanza paparazi wetu alishuhudia kapo hiyo, ilimbidi kusubiria hadi mwisho wa muziki wao na kuwafuata kwenye meza waliyokuwa wametulia.

Licha ya kufichaficha wakati mwingine wakikataa kupigwa picha, mwishowe Papii alikubali kwa kuachia cheko na kuanza kumuelezea mrembo huyo kwamba ni mtu wake wa karibu.

“Huyu ni kama rafiki yangu wa karibu, siwezi kusema ni mpenzi hapana! Yaani ni kama sister (dada) yangu,” alisema Papii.

 

Alipobanwa zaidi kuhusiana na jina lake na alivyokutana naye, Papii alijibu kwa kifupi na kumzuia asiongee chochote;

“Kama unataka jina anaitwa Clarister Mbombo, huyu ni mtoto wa mwanamuziki Mbombo wa Mbomboka (aliwahi kutikisa na Bendi ya Safari Sound miaka ya 1970).”

STORI: Richard Bukos, Risasi Jumamosi


Loading...

Toa comment