The House of Favourite Newspapers

KOLABO 10 KALI ZA MAHABA ZA KUKUMBUKWA

MUZIKI wa Bongo Fleva, unazidi kutafuna miaka kadiri siku zinavyosonga mbele na ngoma nyingi sana zimesikika katika safari ya muziki huu mpaka hapa ulipofika.  

 

Si vibaya leo, tukikumbuka tulipotoka. Hapa chini nimekuandalia ngoma kali za kimahaba, zilizowahusisha wanamuziki wa kiume na kike ambazo zilikuwa ni ngoma za taifa kutoka na kuwafikia mashabiki wengi na kuzikubali.

 

CAZ T FT. MISS SARAH- NAKUHITAJI

Hii ni miongoni mwa kolabo ya mwanzo kabisa ya kimahaba wakati muziki huu wa Bongo Fleva umeanza kasi ambayo ilibamba sana. Wimbo huu kuna watu unawakumbusha wakati wapo darasa la pili, kuna wengine unawakumbusha rafiki zao enzi wanafanya shughuli za umachinga au wapenzi wao wa mwanzo kabisa. Wengine tunakumbuka enzi zile za kuandika nyimbo kwenye madaftari na kutunza stika za wachezaji kina Babangida na Babayaro!

 

K LYNN FT SQUEEZER- CRAZY OVER YOU

Ukimuona kwa sasa Jacqueline Mengi kwenye projekti ‘siriazi’ akizungumzia biashara au kuisaidia jamii unaweza kufikiri hata hakuwahi kuwa mwanamuziki wa Bongo Fleva. Lakini ukweli ni kwamba mwanadada huyu mwenye haiba ya upole alikuwa hatari na wakati anatoa wimbo huu alikuwa ‘on fire’ yaani hakamatiki. Squeezer naye usiseme, unajua kuna wakati unaweza kutamani enzi zijirudie na tuendelee kusikiliza muziki mtamu kutoka kwa wasanii hawa.

 

MEZ B FT. RAY C – KAMA VIPI

‘Tidi..tidi..tidi…’ ndivyo biti la wimbo huu linavyoanza, yaani kama linashitua hivi mazee, halafu Mez B anapanda nalo kabla Ray C hajampokea.

‘Men’ ilikuwa ni hatari sana wakati huo. Ilikuwa ni 2006 hivi, ‘binti’ Ray C, kiuno bila mfupa analainishwa na mistari ya Mez B alipomtajia Wanachemba watakuwa tamashani. Ilikuwa ni bonge ya ‘joint’ kwani Noorah alishiriki pia kwenye wimbo huu. ‘R.I.P’ Mez B, gemu la Bongo Fleva bado linakumis pia.

 

JULIANA KANYOMOZI FT. BUSHOKE -USIENDE MBALI

Wimbo f’lan hivi wa kubembeleza. Moja ya kolabo kali za muda wote za mahaba zilizounganisha nchini mbili, Tanzania na Uganda. Wimbo huu pia kuuacha kwenye listi hii ni sawa na kutenda dhambi!

 

TEMBA FT RAY C – NIPE MIMI

“Wacha moto uwake…wacha moto uwake…mid night…mid night mida mibaya…hahahaaaa…ni rah asana.”Temba enzi hizo alikuwa anajiita kachaa na kwenye wimbo huu alikuwa anauza maneno kwa mrembo Ray C ambaye anaingia kwenye listi hii kwa mara nyingine. Hili nalo lilikuwa ni kolabo la kibabe kuanzia audio mpaka kichupa na wakati huo Kundi la Wanaume Family lilikuwa pamoja likimsapoti Temba kwenye kichupa.

 

SAIDA KAROLI FT BANANA ZORO-NAKUPENDA

Kuna wakati nikisikiliza wimbo huu huwa najiuliza hivi Saida Karoli hajatoa wimbo mwingine mapaka leo? Najikuta nikijiuliza siyo kwa sababu sifahamu nyimbo zake nyingine, la hasha! Bali kwa sababu ya utamu wa wimbo huu. Wimbo huu ni bonge ya kolabo ya nyimbo za mahaba kuwahi kutokea Bongo. Listi ya nyimbo hizi ningekuwa ninaipa namba basi wimbo huu ningeupa namba moja, narudia kusema lilikuwa ni bonge la kolabo.

 

MATONYA Ft. LADY JAY DEE- ANITA

Prodyuza Dunga wa 41 Records wakati huo alikuwa kwenye ubora wake. Ilikuwa ni 2007 na Matonya aliingia kwenye gemu kama ‘kichaa’ hivi na kuliteka na wimbo huu. Dada yake Lady Jaydee alimpa sapoti ya nguvu!

 

AT FT. STARA THOMAS- NIPIGIE

AT anaingia kwenye listi hii na ngoma yake ya Nipigie akiwa na Stara Thomas. Binafsi inanikumbusha wakati namaliza kidato cha nne, mwaka 2010. Wewe sijui inakukumbusha wapi, lakini ukweli unabaki kuwa ukweli mzigo huu ulikuwa mtamu balaa.

 

BARNABA FT PIPI- NJIA PANDA

Ukitaja kolabo za kizazi cha sasa za kimahaba zilizoliteka gemu huwezi kuacha kuutaja wimbo huu wa Njia Panda. Barnaba na Pipi walikuwa wanatengeneza ‘chemistry’ ya ukweli sana.

 

DIAMOND PLATNUMZ FT. HAWA-NITAREJEE

Huu ni wimbo uliosukwa pale Sharobaro Records enzi hizo Diamond na Bob Junior ni washikaji wa kufa na kuzikana. Hii nayo ilikuwa kolabo nzuri na ilimtambulisha Diamond vyema sana kwenye gemu baada ya ngoma zake za mwanzo ukiwemo Wimbo wa Mbagala.

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.