The House of Favourite Newspapers

‘Krismasi Njema’ itakavyosikika duniani Jumapili hii!

christmas-at-beamish-209 Makala na Walusanga Ndaki

WAKATI Waswahili siku ya Jumapili ijayo, siku ya Krismasi tutatakiana heri ya Krismasi kwa maneno ‘Krismasi Njema’, katika ulimwengu wa Kiingereza salam hizo zitakuwa ‘Merry Christmas!’ au ‘Happy Christmas!’

Ukitokea kuwa Ufaransa, basi jitayarishe kusikia maneno ‘Joyeux Noel’. Maneno hayo hutamkwa ‘Zhwaye Noel’.   Usibabaike, yanamaanisha ‘Krismasi Njema’, ni kwa vile kwa Wakristo Sikukuu ya Krismasi hufahamika pia kama Noel.

Bara la Arabuni, salaam za Krismasi zitakuwa ni ‘Milad Said’, yanatamkwa kama yalivyoandikwa.  Ukiwa Norway utawasikia wakipeana salaam za Krismasi kwa maneno ‘Gledelig Jul’ yanayotamkwa ‘Gledelig Yul’.

christmas-xmas-christmas-tree-decorationKatika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu na sehemu za Tabora, kwa Wasukuma, siku hiyo utamsikia mwanamke wa Kisukuma akimwambia mwanamke mwenzake: ‘Makilisimasi gawiza, mayu!’ akimtakia Krismasi njema, au ‘atabadili gia’ na kusema ‘Krismasi soga, mayu!’  Ataongeza utamu na kusema tena: ‘Krismasi nyiza, mayu!’

Ndivyo watakavyosema Wasukuma zaidi ya milioni 12 wanaoongea lugha kubwa zaidi nchini ikifuatiwa na Kiswahili; ni kwa vile Wasukuma wengi hawaongei Kiswahili.

Nchi yenye Waislam wengi zaidi duniani haiko Uarabuni, iko Asia; ni Indonesia! Wakati wa Krismasi Wakristo wa huko husalimiana kwa ‘Selamat hari Natal!’ Yanatamkwa kama yalivyoandikwa.

Visiwani Hawaii, Marekani, eneo la watu wa asili ya Wahindi Wekundu watasema: ‘Mele Kalimaka!’  Itamke ilivyoandikwa.

Waluguru wa Morogoro Jumapili watasema ‘Krismasi Inoghire!’ wakimaanisha ‘Krismasi Njema’. Kwa wanaopenda vitu vitamu, maneno hayo yatamaanisha ‘Krismasi Iwe Tamu Kwako!’

Ukiwa Kagera na Mhaya akakuambia: ‘Wihuka na Krismasi,’ usishangae maana anakutakia Krismasi Njema; mpe zawadi au tabasamu.

Nchi ya Warumi, yaani Italia, makao makuu ya Wakatoliki duniani, wao watasema ‘Buon Natale’ wakitakiana Krismasi Njema.

Hebu kisia, maneno ‘Froehliche Weihnachten’ ni ya lugha ipi? Ni ya Kijerumani yanayomaanisha ‘Krismasi Njema’.  Matamshi yake magumu, ni (Frolike Vinachten). Tofauti na yalivyoandikwa!

Nchini Finland, nchi ya watu wapole, wao watasema ‘Hauskaa Joula’ yanayotamkwa ‘Hoska Yula’.  Majirani zao – Sweden – watasalimiana kwa ‘God Yul’ yanayotamkwa ‘Gudt Yul’, tofauti na ilivyoandikwa.

Wazulu wa Afrika Kusini, watasema ‘Jabulela Ukhisimusi’ ambapo nchini Lesotho watasema ‘Kereseme e Monate’ wakimaanisha Krismasi Njema.

Wajapan wanaotutengenezea magari ya Toyota, Nissan, Fuso na kadhalika, wanachekesha kidogo kwa kusema ‘Kurisu Masu Wo Iwaimasu’.

Wagiriki ni wana wa Adam wenye maneno matamu zaidi ya kupongezana kwani husema: ‘Kalla Xristouyena’ yanayotamkwa ‘Kala Kristoyena?’  Usibabaike; herufi ‘X’ hutamkwa kama ‘K’!

Nchini Uholanzi, kwao na aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm, Jumapili watasema ‘Vrolijk Keerstfeest’ ambayo hutamkwa ‘Vrolik Kersfist’.

Mabingwa wa kucheza filamu barani Afrika, Waigbo wa Nigeria wao husema ‘Ezi Ekeresimesi’ na ndugu zao Wayoruba husema: ‘Ikini oduni Keresimesi’.

Je, unajua nyumbani kwa mwanasoka wa Barcelona, Neymar, huko Brazil na kwa mwanasoka wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo huko Portugal, wote wanaongea Kireno?

Wabrazil ni Wareno waliohama zamani kutoka Ureno wakaishi waliko sasa baada ya kuwaangamiza Wahindi Wekundu, wakazi asilia wa sehemu iitwayo leo Brazil!  Hivyo Brazil na Portugal watasema: ‘Boas Festas’,  inatamkwa kama ilivyoandikwa.

Yote kwa yote, Gazeti la Ijumaa linawatakia wasomaji na Watanzania wote Krismasi Njema!

Kamanda Mpinga; Madereva Zaidi ya 280 Tayari Tumewafikisha Mahakamani

 

Comments are closed.