The House of Favourite Newspapers

KUCHELEWA KUZAA KUNAVYOSABABISHA UVIMBE KWENYE KIZAZI

0

UVIMBE KWENYE KIZAZI

 

 

KUNA aina mbili za uvimbe kwenye kizazi unaoweza kutokea, moja huweza kutokea kwenye mlango wa kizazi na kitaalamu hujulikana kama Cervix na pili sehemu ya ndani ya mfuko wa kizazi ujulikanao kama body of uterus. Sehemu hii ya ndani nayo imegawanyika kutokana na tando za ukuta wa mji wa mimba, kitaalamu huitwa layer of uterus ambapo hushika asilimia kama 75 ya vile vivimbe vyote na mgonjwa akawa na tatizo bila kuonesha dalili zozote.

 

Hii ni kwa vile uvimbe huwa unazuiwa na kuta za kizazi. Sehemu nyingine zinajulikana kama subcerous ambapo ni asilimia 15 na hii husambaa mpaka sehemu ya ndani ya ukuta wa mimba na nyingine hujulikana kwa jina la submicousa hii huchukua asilimia tano na husababisha kubadilika kwa umbo la kizazi na kumfanya mwanamke kujisikia uzito kwenye uvimbe.

 

Aina hii ya uvimbe ni hatari kwani husababisha mwanamke kutokwa damu nyingi lakini pia husababisha maambukizi kwenye kizazi cha mwanamke. Inafaa kuelewa kuwa, fibroids siyo kansa bali ni uvimbe wa kawaida tu ambao hukua kwa kutegemea kichocheo au homoni ya estrogen na ndiyo maana wakati wa kupata uvimbe huo ni kuanzia kubalehe mpaka kukoma kwa hedhi.

 

DALILI ZA UVIMBE KATIKA KIZAZI

Uvimbe katika kizazi cha mwanamke ukiwa mdogo unaweza usiwe na dalili zozote na dalili hutegemea sehemu ulipo na pia ukubwa wake. Dalili za ugonjwa huu mara nyingi ni kutokwa damu nyingi kwa muda mrefu wakati wa hedhi ikiambatana na mabongemabonge isivyo kawaida, au kutokwa damu isiyo ya kawaida katikati ya mwezi au hedhi zisizokuwa na mpango. Maumivu makali ya kiuno hasa wakati wa hedhi na kubana viungo vingine vya mwili pia ni dalili za tatizo hili.

 

Wengine hupata maumivu makali ya tumbo, kuhisi maumivu wakati wa tendo la ndoa, kuumwa mgongo na kwenda haja ndogo mara kwa mara kwani uvimbe hukandamiza kibofu cha mkojo.

 

Tatizo la uvimbe katika kizazi mara nyingi huambatana na maradhi mengine. Maradhi hayo ni kama upungufu wa damu, kufunga choo, matatizo ya figo na mara chache huweza kuwa saratani. Pia uvimbe wa fibroid unapokuwa mkubwa unaweza kusababisha dalili kama mkojo kubaki kwenye kibofu, haja kubwa kuwa ngumu, miguu kuvimba na kupungukiwa damu.

 

MATIBABU

Matibabu ya tatizo hili yanaweza kulenga kutibu dalili au kupunguza uvimbe. Hata hivyo, kama ugonjwa huu hauna dalili unaweza kuwa ukifuatiliwa tu bila kuchukuliwa hatua zozote. Tunapaswa kujua kuwa, mwanamke anapokoma siku zake, tatizo hili nalo hutoweka. Wanawake wengi wana fibroids ndogondogo lakini kwa sababu
hazina dalili huwa hawaendi hospitali na pengine hubainika pale wanapofanyiwa ultrasound.

 

Lakini iwapo watabeba ujauzito, uvimbe huu huongezeka kwa sababu ya vichocheo kuongezeka. Kwa ajili hiyo tunashauriwa kuwa na mazoea ya kufanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara ili kuweza kushughulikia haraka matatizo kama haya.

 

Uvimbe ambao ni mkubwa wenyewe hutibiwa kwa namna zifuatazo:

 

1. Dawa ambazo kwanza ni kwa ajili ya kurekebisha kiwango cha vichocheo vinavyosababisha uvimbe huu na aina ya pili ya dawa ni vidonge vya maumivu ili kutuliza maumivu yanayosababishwa na fibroids.

 

Vidonge vingine vinavyoweza kutumika ni vya kuzuia damu dawa za uzazi wa mpango.

 

2. Njia ya pili ni upasuaji, ambao hutegemea na ukubwa wa uvimbe, pia sehemu ya mfuko wa uzazi ambapo uvimbe upo na wingi wa fibroids. Kuna aina mbili za upasuaji
Myomectomy – Njia hii hutumika ikiwa kuna uvimbe mmoja na si mkubwa sana, na iwapo mwanamke ni kijana anayehitaji kuendelea kuzaa na kwa wale wenye uvimbe mmoja ulio katika sehemu nzuri.

 

Operesheni hii ni kwa ajili ya kutoa uvimbe tu na kuacha kizazi. Hata hivyo katika upasuaji wa aina hii kuna uwezekano mkubwa wa uvimbe kujirudia. Total abdominal hysterectomy – Hii ni aina ya upasuaji ambapo kizazi chote hutolewa na hufanyika ikiwa kizazi kina uvimbe mmoja mkubwa sana au vivimbe vingi.

 

Siyo vibaya kujua kuwa aina ya upasuaji wa uvimbe katika kizazi hutegemea pia umri wa mgonjwa, sehemu ya mfuko wa uzazi ambayo imeathiriwa na uvimbe huo,aina ya fibroid, idadi ya watoto na maamuzi binafsi ya mgonjwa. Baadhi ya wakati pia hata baada ya kufanyiwa operesheni uvimbe hujirudia iwapo vichocheo vinavyosababisha hali hiyo.

 

NA: MWANDISHI WETU KWA MSAADA WA MITANDAO| RISASI

Leave A Reply