The House of Favourite Newspapers

KUPOTEA KWA MTOTO, BALAA LA MGANGA USIPIME!

DAR ES SALAAM: Majanga! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya sakata la kupotea kwa mtoto Gabriella Kilimba (3) kuchukua sura mpya ambapo mganga mmoja jijini Dar amezua kimbembe huku baba na mama pakichimbika, Risasi Mchanganyiko limeshuhudia.

Mtoto Gabriella alipotea miezi miwili iliyopita akiwa amelala ndani nyumbani kwao Ukonga-Mazizini, Dar baada ya mama yake mzazi kwenda hospitali iliyopo jirani kuchomwa sindano.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mama wa mtoto huyo, Tatu Mohammed alisema kuwa tangu mwanaye apotee mpaka sasa imetimia miezi miwili lakini haelewi cha kufanya zaidi ya kumuomba Mwenyezi Mungu.

“Yaani mpaka sasa hivi naishi kutokana na Mungu tu kwa kweli kwa sababu tangu mwanangu apotee ni miezi miwili sasa nimekuwa na sintofahamu kwa kuwa siku hiyo nilienda hospitali nilikuwa na sindano za masaa, ilikuwa saa kumi na moja jioni, nimemuacha mwanangu ndani amelala, niliporudi sikumkuta,” alisema mama huyo.

 

MGANGA AZUA KIMBEMBE

Mama huyo aliendelea kueleza kuwa kutokana na kumsaka mtoto huyo kwa muda mrefu bila mafanikio, wananchi wa mtaa huo walikaa kikao na kutoa maamuzi ya kumtafuta mganga wa kienyeji na kweli akawa amefika kwa ajili ya shughuli maalum.

“Mganga amefika kama hivi unavyoona ametuambia mtoto yupo Zanzibar, alipelekwa kwa njia ya ushirikina lakini anajitahidi ili aweze kurudishwa kwa hiyo nazidi kumuomba Mwenyezi Mungu ili mwanangu aweze kurudi,” alisema Tatu.

 

BABA, MAMA PACHIMBIKA

Kutokana na mtoto kupotea kwa muda mrefu, baba na mama wamejikuta wakiwa na mgogoro mkubwa kila mmoja akimshutumu mwenzake kuwa ndiye anayejua mtoto aliko.

“Habari zinadai baba wa mtoto ndiye amemchukua mwanangu kishirikina kwa kuwa anataka mali na ukizingatia sikuwa na maelewano naye vizuri na tulishatengana hadi matumizi alikuwa haniletei tena, nilikuwa namlea mwanangu mimi na familia yangu,” alisema mama mtoto.

 

Kwa upande wa baba mzazi wa Gabriella, Kilimba Geoffrey aliposhushiwa madai ya mkewe kuwa yeye ndiye anayejua mtoto alipo kwani amemchukua kishirikina alisema hawezi kufanya hivyo.

“Siwezi kufanya hivyo kwa mtoto wangu, kama wanasema nimemchukua kishirikina ili nipate mali sijui ila kuna taarifa ambazo zimenifikia kuwa mama yake mke wangu, yaani bibi wa mtoto anajua kila kitu kuhusu mwanangu maana ana mambo ya kilozi.

“Ninachotaka ni mwanangu arudishwe kwa kuwa na mimi ni mmojawapo niliyefanya huyu mganga aweze kuja hapa, sijaridhika na upoteaji wa mwanangu,” alisema Kilimba.

 

MGANGA AFUNGUKA

“Huyu mtoto anarudi kwa sababu hii kazi niliyoifanya hapa ni kubwa, yaani ndani ya wiki hii lazima mtoto awe amerudi kwa kuwa amechukuliwa kishirikina na yupo Zanzibar anataka kubadilishwa kwa ajili ya ufreemason na ni watu wengi tu wamepotea nimewarudisha nimefanya hii kazi kwa miaka mingi,” alijitapa mganga huyo.

Mtoto Gabriella alipotea mwezi wa tisa ambapo wazazi wake walitoa taarifa polisi na kufunguliwa jalada la kesi lenye namba MAZ/ RB/1349/2018 TAARIFA YA KUPOTEA MTOTO.

Stori: NEEMA ADRIAN, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.