The House of Favourite Newspapers

Mjane Moro afanyiwa kitu mbaya

MOROGORO: Baada ya mumewe ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani hapa, Nyakatale Alphonce kufariki dunia miezi minne iliyopita, mjane ambaye ni mke wake mdogo wa marehemu, Koliden Msindi amedai kufanyiwa kitu mbaya na mke mwenzake aliyemtaja kwa jina la Velena.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mama huyo alisema hivi karibuni aliitwa kwenye kikao cha familia ya marehemu na kupokea kichapo huku akiwa na ujauzito alioachiwa na marehemu, jambo ambalo limemhuzunisha sana.

 

“Juzi wameniita kwenye kikao cha familia, mmoja wa watoto wa mke mwenzangu aitwae Franswasa alinihoji kwamba nilikuwa naishi vipi na baba yao, swali hilo sikulipenda nikaamua kutojibu ndipo nikaanza kushushiwa kipigo na watu waliokuwa kwenye kikao akiwemo mke mwenzangu wakidai mimi ni jeuri,” alidai mama huyo.

 

Mbali na kipigo pia mke mwenzake aliyetajwa kwa jina la Velena ambaye ndiye mke mkubwa wa marehemu alimfukuza kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na sasa analala nje na watoto wake watatu.

“Mimi na Mzee Nyakatale tulianza uhusiano miaka saba

iliyopita na tumejaaliwa kuzaa watoto watatu na ameniacha na ujauzito wa miezi sita.

“Nilikuwa naishi naye kama mke na mume ingawa hatukufunga ndoa ila sehemu ya mahari alishalipa, tulikuwa tuko kwenye mchakato wa kufunga ndoa ya kimila kwa kuwa tayari yeye alikuwa na ndoa ya kanisani ambayo haina talaka japo alikuwa ametengana na mkewe kwa muda wa miaka 10 iliyopita.

 

“Tukiwa kwenye mchakato huo baba watoto wangu ambaye ana migodi ya madini kule Matombo na anamiliki nyumba pamoja na gesti alifariki dunia,” alidai.

Mama huyo aliendelea kutiririka kwa huzuni kuwa kilichomshangaza ni kwamba baada ya arobaini kupita mke mwenzake alimtimua kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na marehemu.

Kutokana na manyanyaso hayo mama huyo alisema aliamua kwenda kwa wanasheria kuomba msaada wa kisheria ili waweze kumsaidia aondokane na mateso anayoyapata na watoto wake hao wadogo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Morogoro Paralegal Centre kinachojihusisha na kutetea wanawake na watoto, Flora Masoy alithibitisha kupokea malalamiko ya mwanamke huyo.

 

“Kweli amekuja hapa ofisini na kutueleza malalamiko yake akiomba msaada wa kisheria.

“Nashindwa kueleza sana jinsi tutakavyomsaidia maana hapa ni mpaka niende mahakamani nikajue msimamizi wa mirathi pia nijue mke wa kwanza alipewa talaka au la,” alisema mkurugenzi huyo.

Ili kuleta usawa wa habari, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta mke mkubwa, Velena na aliposomewa malalamiko hayo dhidi ya mke mwenzake alijibu;

 

“Kwanza huyo ni kama mtoto wangu siwezi kujibishana naye, ni kweli nilimuondoa pale gesti kwa kuwa alishapewa sehemu ya kuishi kule Mvomero, katoka kaja kuishi nyumba ya biashara inayoniingizia kipato hata kama ni wewe usingekubali.

“Alipoondoka kwa kuwa ana watoto wa mume wangu, nilimpa laki tano, alitakaje tena?”

Alipoulizwa kama marehemu mumewe alimpa talaka enzi za uhai wake na kama ni kweli alimpiga mke mwenzake huyo kwenye kikao cha familia mama huyo alijibu;

 

“Mimi ndiyo msimamizi wa mirathi na muda huu natoka mahakamani kufuatilia mirathi hiyo, kama ningepewa talaka ningeteuliwa kusimamia mirathi? Je, ndoa ya Kikristo ina talaka?

“Kuhusu kupigwa kamuulize vizuri akuambie nani alimpiga na kwa nini alipigwa. Je, alienda polisi?”

Stori:DUNSTAN SHEKIDELE, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.