The House of Favourite Newspapers

Kwa nini usiwe mstahimilivu kwa mumeo hadi unachepuka?

0

sex-habits-of-super-happy-couplesKWANZA nianze kwa kuwasalimu wapenzi wasomaji wangu wa kona hii, assalamu alaykum na kwa wale wagonjwa ugueni pole na tuzidi kuombeana.

Baada ya kuwaeleza hayo, niingie moja kwa moja kwenye mada yetu ya leo iliyobeba kichwa cha habari, kwa nini usiwe mstahimilivu kwa mumeo hadi unafikia hatua ya kuchepuka?

Siku hizi wanawake wengi walio ndani na nje ya ndoa wameyageuza mapenzi kama vile fasheni, wanaishi katika ndoa vizuri lakini mwenza wake akipata matatizo kidogo tu anaamua kuanzisha tabia ya kuchepuka na wengine.

Mada hii imekuja baada ya msomaji mmoja kutoka Tanga ambaye amekuwa akifuatilia sana mada zangu kupitia gazeti hili hadi kwenye runinga, hebu msikie kaka huyu;

“Nakupongeza sana kwa mada zako tamu unazotoa katika gazeti la Amani. Mimi ni kijana mfungwa katika gereza moja huku Tanga. Kwanza nashukuru siku hizi tunapewa fursa ya kufuatilia magazeti na kuangalia TV japo ni kwa vipindi maalum.

“Hadi sasa nina miaka mitatu tangu nimefungwa na sababu kubwa iliyonifanya kuwasiliana na wewe ni mke wangu ambaye nimemuacha uraiani. Bi. Chau siku zote maneno ya kuambiwa huwa yanauma sana. Mke wangu ni mmoja kati ya wale wanawake waliopitia vitu muhimu ambavyo ni Usinga, Kibwaya na Njuga kifupi ni mwanamke aliyefundwa.

“Mwanzoni tulikuwa tukipendana sana lakini tangu nimefungwa amebadilika kila kitu, nimekuwa nikisikia habari nyingi za kuniumiza. Amekuwa mchepukaji maarufu ni wa kutembea na wanaume tofauti kila kukicha, imeniuma sana na ndiyo maana nimekushirikisha kwa kuwa ndiyo kwanza namalizia kifungo,” alimaliza kusema msomaji huyo.

Kwanza nimpe pole sana kwa yaliyomkuta. Pili niwageukie wanawake wenzangu na kuwauliza hivi mumeo akipata tatizo kidogo ni lazima uchepuke? Tabia ya wapi hii?

Tabia hii imekuwa ikijijenga sana kwa wanawake wenzangu na siyo tu kwa wale waume zao waliopo gerezani wakati mwingine hata wakiwa hoi kitandani wanaumwa na wakishamaliza shida zao baada ya kuchepuka wanaishia kusema ohh eti shetani alinipitia. Jamani tubadilike, jambo la msingi na liwe somo kwa wengine leo ni kuwa mstahimilivu katika mapenzi, mpende na mthamini mwenza wako tangu siku ya kwanza kujuana mpaka siku ya kuzikana, kusameheana ni jambo jingine jema katika mapenzi.

Kwa leo naishia hapa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Leave A Reply