The House of Favourite Newspapers

Lazima Wakenya Wakae Leo!

starsWAKATI leo Alhamisi kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kikishuka kwenye mechi yake ya pili ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mbele ya Kenya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametamba kwamba Kenya lazima wapigwe.

Makonda aliyasema hayo wakati alipotembelea jana kambi ya Stars jijini hapa wakati ikiwa inajiandaa na mechi hiyo na Kenya. Stars inayofundishwa na kocha Emmanuel Amunike leo Alhamisi itacheza mechi yake ya pili ya Afcon baada ya ile ya kwanza kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Senegal.

 

Makonda alitua Misri jana baada ya kumuomba Rais John Magufuli kuja kuongeza hamasa kwa timu hiyo huku akiamini uwepo wake utachangia Stars kushinda.

 

Akizungumza wakati yupo kambini hapo, Makonda amesema amewakuta wachezaji wa Stars wana ari ya juu na wameahidi ushindi mbele ya Kenya. “Wakenya kesho (leo) lazima wakae, nimekutana na wachezaji na wapo kwenye ari ya juu sana.

 

“Kipigo ambacho tuliwapa Uganda ndiyo hicho ambacho tutawapa, kwenye michuano hii sisi tumekuja kufanya kazi, tutashinda mechi hii na nyingine zinazofuata na ikiwezekana tutatwaa ubingwa,” alisema Makonda.

Naye Amunike amefunguka kuwa, lazima washinde mchezo wa leo mbele ya Kenya ingawa anaamini hautakuwa mchezo rahisi. Amunike ametoa kauli hiyo wakati leo timu hizo zitakapopambana kwenye Uwanja wa Juni 30 uliopo Cairo nchini Misri ukiwa ni mwendelezo wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika.

 

Taifa Stars baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Senegal kwa mabao 2-0, leo itakuwa na cha kujiuliza mbele ya Kenya ambayo nayo ilifungwa na Algeria kwa idadi hiyo ya mabao.

 

Kocha huyo alisema wataingia kwa tahadhari kubwa kuona wanafanya vizuri kwenye mchezo huo ambao kila upande umeutolea macho. Amunike amesema kutokana na wachezaji wake wote kuwa fiti tofauti na ilivyokuwa mchezo wa kwanza, anaamini watafanya vizuri na kujenga sura mpya ya kundi hilo ambalo Algeria na Senegal wanaongoza wakiwa na alama tatu kila mmoja.

 

“Tunaenda kukutana na mechi ngumu dhidi ya majirani ambao lugha inayozungumzwa ni moja, kila mmoja anahitaji kushinda ili kuwa kwenye nafasi nzuri.

 

“Lakini kwa upande wetu kama timu, tumejipanga na wachezaji wangu kwa asilimia kubwa wale ambao hawakuwa fiti awali kwa sasa wapo vizuri. Lazima twende kwa tahadhari kubwa kwani wapinzani wetu siyo wabaya.

 

“Ila kikubwa ni sapoti kutoka kwa Watanzania na watambue kwenye soka kuna matokeo ya aina tatu, kushinda, sare au kufungwa kikubwa tumejipanga kuibuka na ushindi kuliko kitu kingine chochote,” alisema Amunike, ambaye alitwaa taji hilo la Afrika wakati akichezea Nigeria kwenye michuano iliyofanyika mwaka 1994 nchini Tunisia.

Comments are closed.