The House of Favourite Newspapers

Ligi Ni Ngumu, Lakini Kilichowabeba Yanga Dhidi Ya Kagera Ni Hiki Hapa

Kikosi cha timu ya Yanga.

JUZI Jumamosi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa katika Uwanja wa Kaitaba uliopo mjini Bukoba mkoani Kagera. Katika mchezo huo, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu ndiyo walioifungia Yanga mabao mawili, huku lile la Kagera likifungwa na Jaffar Kibaya.

 

Haikuwa rahisi kwa Yanga kupata ushindi huo ugenini, lakini ngoja nikwambie kikubwa ambacho kilichoibeba timu hiyo inayonolewa na Mzambia, George Lwandamina. Yanga imekuwa ikicheza vizuri sana kwenye viwanja ambacho vina sehemu nzuri ya kuchezea. Miongoni mwa viwanja hivyo ni Taifa, Uhuru, Azam Complex na Kaitaba. Mbali na hivyo, vilivyobaki vyote havipo vizuri.

 

Ukiangalia Uwanja wa Kaitaba, ulikuwa ukiwaruhusu Yanga kucheza wanavyotaka na kujiona kama walikuwa nyumbani, hiyo ndiyo sababu kubwa iliyowafanya kuibuka na ushindi huo ujapo si mkubwa sana. Ushindi ni ushindi tena hasa ukiwa ugenini unatakiwa kujivunia kwani timu nyingi zimekuwa zikipoteza zikienda ugenini tofauti na zinapokuwa katika viwanja vyao vya nyumbani.

 

Hivi sasa Yanga inakwenda Shinyanga kucheza na Stand United ambapo mchezo wao utapigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani humo. Uwanja huo ni mmoja kati ya viwanja vinavyolalamikwa kwamba havina ubora sehemu ya kuchezea. Mchezo huo ujao kwa Yanga ndani ya Uwanja wa Kambarage, unaweza kuwa mgumu kwao kutokana na hali ya uwanja ilivyo.

 

Tuliona Simba ilipokwenda kucheza na timu hiyo uwanjani hapo, ilipata ushindi wa 2-1 lakini kwa tabu sana. Sasa Yanga sijui itakuwaje. Tukiachana na hilo, wiki iliyopita nilisema kwamba mechi za wikiendi hii zitakuwa na ushindani mkubwa na zinaweza kubadilisha kabisa sura ya msimamo wa ligi hiyo na kweli ikawa hivyo.

 

Waliokuwa juu wameshuka na wale waliokuwa chini wamepanda. Hiyo yote ni kudhihirisha kwamba hakuna timu ya kuibeza kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16. Tumeona ushindi wa Yanga juzi, uliwafanya kukaa kileleni wakifikisha pointi 12. Hiyo ni kabla ya jana Simba haijapambana na Mtibwa Sugar. Mechi zingine za wikiendi tuliona Singida United ambao walianza vizuri, wamepata sare dhidi ya Ruvu Shooting, huku Azam nao ambao walikuwa wakipambana na Mwadui, wakitoka sare.

 

Ndanda na Majimaji zilitoka 1-1, huku Njombe na Lipuli zikishindwa kufungana. Ugumu huo wa ligi unanifanya niendelee kuamini kwamba msimu huu bingwa hawezi kutabirika mpaka sasa, tunasubiri kuona huko mbele itakuwaje. Msimu uliopita tulishuhudia Yanga ikichukua ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba, jambo kama hilo linaweza kutokea kwa msimu huu pale atakapoamuliwa bingwa, lakini inaweza kuwa zaidi ya hivyo, yaani zaidi ya timu mbili zikafungana pointi kutokana na hiki kinachotokea sasa.

Edibily Lunyamila Mawasiliano +255 713 507 097

Comments are closed.