The House of Favourite Newspapers

Lissu Ashuhudia Gari lake Polisi, Ataka Waliompiga Risasi Watafutwe.. Akanusha Uvumi wa Kuzuiwa Kuliona

0

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameliomba jeshi la polisi nchini kuendelea kumsaka aliyehusika na shambulio dhidi yake na kumshughulikia kwa mujibu wa sheria.
Lissu ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Mei alipofika katika kituo kikuu cha Polisi Dodoma kuona gari alilokuwemo pindi aliposhambuliwa tarehe 7 Septemba 2017 katika eneo la Area D jijini Dodoma.

Lissu amefika kushuhudia gari hilo kwa mara ya kwanza ikiwa imepita miaka sita tangu ashambuliwe na kusema kuwa lina matundu ya risasi 30 ambayo yote yalimlenga mtu mmoja ambaye ni yeye.

Akizungumza na waandishi wa habari amesema; “Nilifanya mawasiliano na uongozi wa Jeshi la Polisi Dodoma nashukuru wameniwezesha kuliona, nimehesabu matundu ya risasi yapo 30, imenifikirisha sana kwamba risasi zile zilizoelekezwa kwa mtu mmoja ni unyama wa hali ya juu,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya kukamilisha nyaraka muhimu atachukua gari hilo ili maisha mengine yaendelee.

Kuhusu maneno yaliyopo kwamba polisi walizuia gari hilo Lissu amesema huo ni uvumi na kwamba hakuna siku aliyowahi kukatazwa na jeshi hilo kuona gari lake.

“Kuchukua hii gari sio kwamba naondoa au nafuta kesi, kulingana na sheria za Tanzania kesi za aina hii zinahesabika kama jinai, kesi hízi huwa mali ya Jamhuri, sina uwezo wa kuamua kesi ifanyike au isifanyike zaidi ninatumika kama shahidi tu!” amesisitiza.
Mbali na hayo mwanasiasa hiyo amekanusha tuhuma za kukataa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kuhusu kushambuliwa kwake na kusema hajawahi kufanya hivyo kwani anaelewa hilo ni kosa la jinai na halikubaliki kisheria.

“Puuzeni maneno ya kijingajinga, siku zote nimekuwa nikitoa ushirikiano kwa polisi na hadi sasa natamani huyo aliyenipiga risasi zote hizo atafutwe na ashughulikiwe kisheria,” amesema.

Kuhusu kuingia na kutoka nchini mara kwa mara ameeleza kuwa ni kawaida yake na kwamba suala hilo lisichukiliwe kama ni hofu ya usalama wake.

“Nafanya kazi za kimataifa, safari zangu zipo vilevile kama ilivyokuwa mwanzo. Jumamosi iliyopita nilitoka Ulaya na mwezi ujao nitaenda mara mbili Ulaya ni kawaida isichukuliwe kitofauti” amesema.

Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti huyo amezungumzia kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya kuwa kinachoendelea ni maneno tu na hakuna vitendo.

Amesema ili wao wamuamini Rais Samia Suluhu Hassan, wanahitaji kuona matendo zaidi kuliko maneno.

Kuhusu mahali aliko dereva ambaye alikuwa naye wakati anashambuliwa, Lissu amesema yuko nchini Ubelgiji na kwamba alipelekwa huko kutokana na sababu za usalama wake kuwa kwenye mashaka.

“Dereva wangu nilienda naye Ubelgiji, amelowea huko na kujua lugha zaidi yangu, maneno kwamba amekimbia nchi yake ni ya kijinga muda wowote akitaka atarudi, hapa ni kwake,” amesema.

Leave A Reply