The House of Favourite Newspapers

Luiza Mbutu Mkongwe anayezeekea Twanga

0

LuizaMbutuLuiza Nyoni Mbutu

Stori: MAYASA MARIWATA

LUIZA Nyoni Mbutu ni miongoni mwa wasanii wakongwe wa muziki wa dansi, ambaye haikuwa kazi rahisi mpaka kufika hapo alipo kutokana na changamoto mbalimbali alizopitia.

AMEANZIA MBALI
Akizunguzia safari yake ya kimuziki, Luiza ambaye ni mzaliwa wa Jiji la Dar, alisema alijikita rasmi kwenye shughuli hizo mnamo mwaka 1996 katika Bendi ya Air Jaz ambayo ni ya Jeshi la Anga kwa ushawishi mkubwa wa dada ambaye naye alikuwa mwanamuziki, Modesta Nyoni yeye wakati huo alikuwa akiitumikia Twiga Band.

KANISA, FAMILIA VILIMPINGA
Haikuwa kazi rahisi kukubalika katika fani hiyo hususan kwenye familia yake ambapo alikuwa akiishi na mjomba wake maeneo ya Sinza-Palestina jijini Dar na kumpiga vita kila kukicha katika suala hilo kwa kuamini ni uhuni.

Kama hiyo haitoshi, kanisa alilokuwa akisali, Kanisa Katoliki Parokia ya Sinza nao hawakukubaliana naye, waliona kama anawadhalilisha japo baadaye waliamua kumuacha asake ridhiki kwa upande huo.

KTMA15“Haikuwa rahisi mpaka kufika hapa nilipo kuna watu wengi walinipiga vita, hata hivyo sikudumu kwenye bendi hiyo kwa kuwa walikuwa wanataka watupe ajira ya kudumu lakini mambo yao yakaenda sivyo wakaghairi, nikahamia Bendi ya Magoma Moto ilikuwa maeneo ya Mwenge.”

AHAMA TENA
“Huko napo sikudumu mwaka uliofuata 1997 nikaacha kwa kuwa muda mwingi tulikuwa tukiimba kwenye hoteli mbalimbali, sasa wakakodisha vyombo alipokuja Ivon Chakachaka lakini wakaingia mgogoro na watu waliowapa ile bendi ikafa,” anasema Luiza.

AJIUNGA TWANGA
Akizungumzia mikimiki aliyokutana nayo hadi kufanikiwa kujiunga na Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ mwaka 1998, Luiza anasema baada ya Magoma Moto kufa, Mkurugenzi wa Twanga, Asha Baraka alikuwa akitafuta wanamuziki ndipo kuna kijana mmoja akamuunganisha naye na kujikita rasmi hadi sasa.

“Nilivyojikita huko tukatoa ngoma ya kwanza ambayo aliitunga marehemu Banza Stone iliitwa Kumekucha, ndipo kwenye kundi wakajiunga Adolf Mbinga na Abuu Semhando tukatoa nyimbo ya Kisa cha Mpemba ndiyo bendi yetu ikapanda chati kwa kuwa hiyo nyimbo ilikuwa gumzo sana.”

Mwanamuziki huyo ambaye ndiye kiongozi wa bendi, alisema tangu hapo wamekuwa wakitoa albamu karibu kila mwaka yenye nyimbo si chini ya saba na yeye akishiriki kwa mchango mkubwa, jambo linalomfanya ashindwe kukumbuka idadi ya nyimbo alizoimba tangu ajikite na bendi hiyo ambayo inakamilisha albamu 13 mpaka sasa.

Aliongeza kuwa wanamuziki wa zamani hawakuichukulia kazi hiyo kama sehemu ya kipato bali ni sehemu ya kuinjoi tofauti na sasa suala la fedha limepewa kipaumbele, japo kuna kipindi muziki huo wa dansi unayumba kwa kuwa muziki ni kama maisha kuna kupanda na kushuka.

CHANGAMOTO
Luiza anasema miongoni mwa mambo magumu aliyopitia ni kushikwashikwa na mashabiki jambo lililokuwa likimuumiza kichwa muda wote kutothaminika kwenye kazi yake kwa kuwa watu wengi kipindi hicho hawakuwa waelewa walikuwa wakiamini wanaofanya kazi hiyo ni wahuni.

“Mara kadhaa nilijaribu kushika spika na kuongea hadharani kuwa sisi si wahuni bali hii ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na muda mwingine mimi na wenzangu tulijaribu kuwatambulisha wapenzi wetu ili kidogo mashabiki waogope na uzuri mpenzi niliyekuwa naye alikuwa muelewa na kunipa sapoti katika kila jambo.”

UHUSIANO
Katika sekta ya mapenzi, Luiza anasema anajivunia kuwa yupo na mume wake mpaka sasa na kabahatika kupata mtoto mmoja wa kiume aliyempa jina la Brian (12), japo miongoni mwa vitu anavyojutia ni kutozaa mapema.

“Nimegundua kuzaa mapema kuna raha yake sasa hivi ningekuwa na watoto wakubwa tu, lakini mara nyingi wanawake huwa tunaona suala la kuzaa halihitaji haraka matokeo yake ndiyo haya unabaki kutamani wenzio wenye watoto wengi na wakubwa ambao wanawasaidia kimaisha.”

MAFANIKIO
Mkongwe huyo wa muziki wa dansi anasema kwa upande wa mafanikio alisema anamshukuru Mungu anaendesha maisha yake vizuri kupitia bendi hiyo ndiyo maana amedumu mpaka sasa, kwa kuwa suala la fedha halimpi mawazo kwa kiasi kikubwa.

Leave A Reply