The House of Favourite Newspapers

LYNN; KUTOKA USWAHILINI HADI KUMILIKI MAGARI 4 YA KIFAHARI

Irene Hillary ‘Lynn’

MAISHA ni safari ndefu, unaweza kuanzia kwenye maisha mazuri ukaishia kwenye mabaya au ya kawaida lakini pia ukaanzia kwenye mabaya ukaishia na mazuri.  

 

Vivyo hivyo kwa mastaa wetu Bongo wapo ambao wameanzia kwenye maisha ya shida na taabu, ya kawaida na wengine walianzia kwenye maisha ya kitajiri. Miongoni mwa mastaa ambao wameanzia kwenye maisha ya kawaida na kuwa juu ghafla baada ya muda mfupi na kuwashtua wengi ni Irene Hillary ‘Lynn’.

 

Lynn ni muuza sura kwenye video za wasanii Bongo ambaye ndiyo kwanza alionekana kwenye Wimbo wa Kwetu wa Msanii Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ ambaye yupo chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na staa wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Lynn amezaliwa na kukulia maeneo ya Buguruni-Rozana jijini Dar es Salaam ambako ni kwa kawaida, hapaendani na maisha yake ya kifa hari aliyonayo kwa sasa ambayo ni ya vurugu mjini licha ya kwamba hana siku nyingi kwenye fani.

MAFANIKIO YAKE

Ana umri wa miaka 18 ila mafanikio yake ni makubwa na ameyapata kwa kipindi kifupi tu ambapo anamiliki, magari na nyumba. Lynn anadai anamiliki nyumba nne za maana maeneo ya Mbezi- Beach na Goba jijini Dar ikiwemo moja ya kifahari ya ghorofa moja anayoishi maeneo ya Goba.

MAGARI ANAYOMILIKI

Anamiliki magari manne ya kifahari ambayo ni BMW Z3 lenye thamani ya shilingi milioni 10 za Kibongo, Volkswagen Touareg lenye thamani ya shilingi milioni 18, Toyota Mark X ambayo ni ya shilingi milioni 10 na Jaguar X-Type lenye thamani ya shilingi milioni 50. Katika magari hayo manne, moja aina ya Volkswagen alipewa zawadi na mtu asiyejulikana siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake iliyofanyika hivi karibuni.

 

ANAZUNGUMZIAJE?

Akizungumza hivi karibuni kuhusu mafanikio yake ya ghafla mpaka kufikia kumiliki magari manne na nyumba, mwanadada huyo alisema kuwa magari hayo ni yake na vielelezo yaani hati zake na za nyumba anazo na amekuwa akizianika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Mali hizo ni zangu na kila ninaponunua gari huwa naweka vielelezo mitandaoni vikiwa na jina langu pia nina nyumba nne, huo ndiyo ukweli sidanganyi, ninajivunia kuwa na mafanikio haya kwa umri mdogo nilionao kwani nimewapita hadi niliowakuta wakiwa juu mjini,” alisema Lynn mwenye umri wa miaka 19. Lynn ni miongoni mwa wasichana ambao wamekuwa wakihusishwa kutoka kimapenzi na mwanamuziki Diamond.

STORI : GLADNESS MALLYA

LOOH! Kumbe Desturi Za Wakurya Zinaruhusu Wanawake Kuoana

Comments are closed.