The House of Favourite Newspapers

MABESTE; AFUNGUKIA UGOMVI NA JUX, MSOTO KWENYE GEMU

Venance ‘Mabeste’

BONGO kuna utitiri wa marapa, tena wenye uwezo mzuri tu wa kusema na kinasa sauti, katika listi hiyo ya marapa ni jambo la kushangaza usipolikuta jina la Mabeste

Venance ‘Mabeste’. Mabeste ni rapa aliyeibuka miaka takribani nane hivi na kukimbiza kwenye gemu na ngoma kali zikiwemo Baadaye Sana na Sirudi Nyuma, ambazo zote alimshirikisha mshikaji wake wa nguvu kipindi hicho ambaye ni mwanamuziki anayekimbiza kwenye gemu la Muziki wa R&B Bongo, Juma Khalid ‘Jux’.

Baada ya kukimbiza na ‘hit song’ kadhaa, kuna muda Mabeste alisizi kidogo kwenye gemu, kusizi kwake kulitokana na matatizo aliyoyapata kwani alikuwa akiuguliwa na mkewe aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo tangu mwaka 2013.

Kwa sasa Mabeste ameachia ujio mpya, ngoma inaitwa Chakusema ambayo imefanywa na Prodyuza Rush The Don huku kichupa kikifanywa na Paxpyne. Star Showbiz, juzikati ilimkaribishaMabeste mjengoni, Sinza-Mori na kupiga naye stori kadhaa, huyu hapa kwenye mahojiano shuka naye mwenyewe;

Star Showbiz: Niaje mzee ulikuwa kimya sana mzazi hata baada ya kupona kwa mkeo nini tatizo?

Mabeste: Tatizo lilikuwa menejimenti. Unajua nilipotoka kimuziki pale B-Hits kila kitu kilikuwa kinafanywa na timu kwa sababu ilikuwa ni menejimenti kubwa, lakini baada ya kuacha kupiga kazi pamoja kila kitu imekuwa ikinilazimu kufanya mwenyewe, ndiyo maana nakutana na ugumu kwenye kazi.

Star Showbiz: Lakini kuna kipindi ulitangaza kwamba mkeo ndiyo meneja wako, kwa nini mambo yasiende, au hafanyi kazi yake ipasavyo?

Mabeste: Si kweli kwamba mke wangu ni meneja wangu. Ni mtu wangu wa karibu ambaye tunasaidiana kwenye kazi. Nilipotoka B- Hits, niliamua kusema kwamba mke wangu ni meneja wangu ili menejimenti nyingi ambazo zilikuwa zinanimezea mate ziwe mbali na mimi.

Sikuhitaji kuingia kwenye menejimenti nyingine kwa haraka kwa sababu nilifahamu pengine ningekutana na mazingira magumu na kudidimia zaidi kimuziki kuliko nilipokuwa B-Hits.

Star Showbiz: Unaweza kuwakumbusha mashabiki wasiyofahamu, nini kilikufanya utoke B- Hits?

Mabeste: Tuligombana. Kuna wakati ulifika kukawa hakuna maelewano mazuri baina yangu na uongozi wa menejimenti hiyo. Kiukweli kwa namna moja au nyingine suala hilo liliniumiza sana. B- Hits nilitoka nao mbali sana. Pancho Latino tumetoana mbali, tulikutana bado mimi ‘underground’ na yeye hajatoka, tukafanya mambo mengi pamoja mpaka kuwa maarufu pamoja na tukiishi kama familia.

Kwa hiyo kugombana kwetu, iliniathiri kwa namna moja au nyingine kimuziki na hata yeye, maana unaweza kuona B-Hits haisikiki kama ilivyokuwa awali.

Star Showbiz: Kuna wakati pia wewe na mshikaji wako Jux mlikuwa hamuivi chungu kimoja nini kilitokea?

Mabeste: Kuna hali ya kutoelewana tu ilitokea huko nyuma na sipendi kuizungumzia sana. Lakini Jux ni mshikaji, tumetoka mbali sana kabla hata hajaenda China kwa ajili ya masomo.

Star Showbiz: Uhusiano wenu upo vipi kwa sasa?

Mabeste: Siyo mbaya. Ninamshukuru, ingawa hatukutani kama ambavyo ilikuwa zamani. Kwa sasa tumekwishakuwa watu wazima, kila mmoja ana majukumu yake, kwa hiyo muda mrefu huwa unapita bila kukutana wala kuwasiliana.

Star Showbiz: Ngoma yako ya mwisho umeitoa kama miezi mitano iliyopita, inaitwa Sijui, una ‘views’ kama elfu sita tu katika Mtandao wa Youtube, unafikiri kazi yako ilifika kwa watu wengi na mahali inapostahili? Lakini hii inajidhihirisha unapitia msoto kwenye gemu?

Mabeste: Kwa namna moja au nyingine ninaweza kukiri haijafika kule ninakohitaji ifike. Lakini ndiyo kama nilivyosema mwanzo ninahitaji timu ya kusapotiana nayo kwenye kazi haya mambo mengine yatakuwa poa tu.

Kuhusu msoto, si kweli. Mimi ninajiona ninasonga mbele. Mabeste wa miaka ya nyuma siyo wa sasa, nimekuwa kiakili na hata malengo ni makubwa kuliko zamani. Kwa hiyo si kweli kwamba ninakula msoto.

Star Showbiz: Mbali na muziki una kipi tena unajishughulisha nacho?

Mabeste: Mimi na mke wangu tunamiliki kampuni ya utalii ambayo tumeiandikisha kwa majina ya watoto wetu. Hii ni kwa ajili ya watoto wetu lakini kwa namna moja au nyingine inatupatia mkate wa kila siku.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.