MADAI MAZITO MUME AMUUA MKE WAKE BAA

MACHOZI! Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Dulla, Mkazi wa Tabata-Matumbi jijini Dar, anadaiwa kumuua mkewe, Aisha Abdallah (34), naye mkazi wa Tabata-Matumbi.  Dulla alisemekana kumpa Aisha kipigo cha hatari wakiwa kwenye Baa ya Matumbi-Tabata jijini Dar kisha kutokomea kusikojulikana ambapo sasa anasakwa na Polisi.

Ilidaiwa kwamba kipigo hicho ndicho kilichosababisha umauti wa Aisha. Habari zilizopatikana eneo la tukio zilieleza kuwa, tukio hilo lililoacha mshtuko na mshangao wa aina yake lilijiri Novemba 14, mwaka huu, majira ya saa 4:00 usiku kwenye baa hiyo.

Ilikuwaje? Mashuhuda wa tukio hilo walilisimulia Ijumaa Wikienda kuwa, wawili hao walikuwa katika baa hiyo ambayo ipo jirani na maeneo wanayoishi ambapo kama kawaida yao walikuwa wakipooza makoo yao baada ya mizunguko ya siku nzima ya kimaisha katika Jiji la Dar. Kwa mujibu wa jirani wa Aisha wanayeishi kwenye nyumba zinazofuatana aliyejitambulisha kwa jina la Mama Azizi, yeye ni mfanyabiashara katika Barabara ya Matumbi na alikuwa na Aisha kabla ya kukutwa na tukio hilo.

“Ulikuwa muda wa usiku, nilikuwa nimekaa na Aisha sehemu yangu ya biashara ya chipsi. “Nakumbuka Aisha aliniuliza kama nimemuona Dulla? Mimi nikawambia Dulla sijamuona. Akaniambia ngoja akae pale kwenye sehemu yangu ya biashara amsubiri.

“Wakati tukiwa pale tuliendelea kupiga stori tu, mara akapita Dulla, Aisha akamuona na kumwambia mbona anampita wakati alimwambia yupo kwangu (kwenye biashara ya Mama Azizi)? “Dulla akaitikia, akamwambia Aisha twende kule juu akimaanisha baa. “Kwa hiyo kilichoendelea kule baa mimi sikijui hadi alipokuja mpangaji mwenzangu na kuniambia Dulla kampiga Aisha mateke ya tumboni na kifuani hadi amezimia.

“Ilibidi nitoke pale kwenye biashara yangu, nikaelekea huko baa. “Kule baa nikamkuta Aisha amelala chini, ndipo tukawa tunampepea wote pamoja na wahudumu wa hiyo baa. “Tulihangaika sana kumnusuru Aisha na umauti ndipo Dulla akapotea pale katika mazingira ya kutatanisha kwani hakuna aliyejua alikoelekea.

“Tukaendelea kumpepea pale maana sisi tulijua amezimia, tukamuagiza mwenzetu mmoja kwa kuwa nyumbani siyo mbali tukamwambia akalete maji ya baridi. “Baada ya kuleta maji ya baridi tukammwagia kwenye miguu na kumkandakanda mikononi, lakini maskini Aisha hakuamka.

“Ndipo ikabidi tuchukue Bajaj kisha tukambeba na kumpakia humo, tukapitia Kituo cha Polisi cha Tabata ambako tulipewa PF-3 (fomu ya matibabu) na kufungua jalada la kesi kisha tukaelekea Hospitali ya Amana (Ilala).

“Tulipofika Amana, daktari alimpima Aisha, akawa anambonyeza maeneo ya kifuani, akatuambia kuwa ameshafariki dunia. “Kiukweli sikuamini kabisa, lakini ndiyo hivyo, tuliporudi Tabata-Matumbi tukaambiwa Dulla alishapotelea kusikojulikana hivyo anasakwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Aisha,” alisema mama huyo.

Kwa upande wake mdogo wa marehemu Aisha aliyejitambulisha kwa jina la Yusuph Abdallah alisema kuwa aliyefanya tukio hilo wao kama familia hawakuwa wakimtambua kwa kuwa hakuwahi kwenda kwao kujitambulisha isipokuwa walikuwa wakisikia tu kuwa Aisha anaishi na mume jijini Dar.

“Mimi ninaishi Morogoro, nilipigiwa simu kuambiwa dada yangu amefariki dunia, ikabidi nije, nilipofika Dar, kwa mujibu wa hawa aliokuwa nao, Aisha alikuwa na huyo bwana ambaye wao wanamtambua kama mume wake, walianza kwa kutaniana.“Niliambiwa walikuwa baa na pale baa walishazoeleka kama watu wanaopenda kutaniana  ndiyo maana hata siku hiyo ya tukio inasemekana walianza kwa kutaniana kama kawaida yao.

“Kila mtu alishangaa kwani hakujua nini kimewatokea, lakini Dulla ilisemekana alimsukuma Aisha, akadondoka na kuanza kumkanyagakanyaga maeneo ya kifua na baada ya kufikishwa hospitalini akawa tayari ameshafariki dunia.

Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamduni ili kuthibitisha tukio hilo simu iliita bila kupokelewa na hata alipoelezwa jukumu la kupigiwa simu kwa njia ya ujumbe mfupi hakujibu. Mwili wa marehemu Aisha ambaye hajaacha mtoto ulisafirishwa Novemba 16, mwaka huu kuelekea Mbalizi jijini Mbeya kwa mazishi huku Dulla akiendelea kusakwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji.

Mmoja wa wataalam wa saikolojia aliyezungumza na gazeti hili juu ya tukio hilo alitoa tahadhari kwa wapenzi wanaokwenda baa kuwa makini linapokuja suala la ugomvi kwani kila mmoja anakuwa na kilevi kichwani hivyo jambo baya linaweza kuwatokea.

WEMA Alivyotinga Mahakamani Tena, Kesi ya Video za Ngono!

Toa comment