The House of Favourite Newspapers

MADAM RITA: ALIPUUZWA NA KUKATISHWA TAMAA, AKAINUKA NA KUTUSUA!

Rita paulsen

KATIKA maisha hakuna mtu anayepanda bila kukanyaga ngazi. Kwa hiyo ili maisha ya binadamu yakamilike, yanatakiwa kupitia njia hizo. Unaweza kupewa mtaji wa kila kitu na ukashindwa kuendeleza.  Mpenzi msomaji wa Gazeti la Ijumaa, hatuwezi kuchoka kukutia moyo. Tumekwishakuletea simulizi mbalimbali za maisha ya watu maarufu ambayo wamepitia mazingira magumu kama pengine unayokutana nayo wewe kwa sasa au zaidi wakati wakipigania ndoto zao, lakini hawakuchoka, walipambana bila kujali ni mazingira gani yanaowakabili mpaka wakafika pale walipo kwa sasa.

Nikikukumbusha baadhi ya simulizi ni ya msanii wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye alikuwa mbali na mikono ya wazazi wake, alifanyiwa kitendo kibaya akiwa binti wa miaka 14, akapata mtoto, akaolewa na baadaye kutimuliwa na watoto. Lakini hakukata tamaa, aliamini kupitia kile Mungu alichomjalia ndani yake akapambana na leo ni mtu maarufu na anaishi maisha yake.

Wapo akina Michelle Obama, Oprah Winfrey, Serena Williams na wengine wengi tumewaleta kwako ili uweze kuona namna ‘struggle’ za kutimiza ndoto zinavyohitaji nia ya dhati.

Sasa kuhusu siku ya leo, ningependa kukumegea vitu vichache kumhusu mwanamama Rita Paulsen ambaye wengi wanamtambua kama Madam Rita kupitia shindano lake la kusaka vipaji vya muziki la Bongo Star Search. Miaka 13 iliyopita, Madam Rita alikuwa ni mwajiriwa katika TV moja kubwa nchini, lakini alifukuzwa na kupata wazo la kuanzisha kampuni yake ya Benchmark Productions akiwa na umri wa miaka takribani 23 tu, kwa nini wewe ushindwe?

Kampuni hiyo alikomaa nayo na ndiyo ikatengeneza njia ya video za muziki za wasanii wa Bongo Fleva kutoka mfululizo zikiwa katika hadhi ya juu. Nikumegee tu, kampuni hii ndiyo iliyomtoa mwanamuziki mkongwe, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ kwa mara ya kwanza kupitia video ya wimbo wake wa Machozi kisha ikatengeneza video ya kiwango ya mwanamuziki Joseph Haule ‘Professor Jay’ iitwayo Zali la Mentali.

HAKUKATA TAMAA

Madam Rita anasema moja kati ya malengo yake maishani ni kutokukata tamaa. Anasema ilifika mahali wakawa wanatengeneza video bila kuwa na faida na ndiyo chanzo cha kusitisha na kuangalia biashara nyingine na ndipo akaibukia kwenye kuandaa Shindano la Bongo Star Search.

“Nilivyokuwa naongelea hilo suala la kuanzisha Bongo Star Search, watu waliokuwa karibu na mimi wakaniambia ‘you are crazy, hiyo shoo ni ya mamilioni sijui ngapi ya dola, huwezi kufanya, kwanza watu hawawezi kujitokeza,” anasema Rita. Anasema baada ya kukatishwa tamaa, wazo hilo aliliweka pembeni kidogo kwa miaka mitatu, lakini aliamua kulisajili kwanza. “Sikuweza kuifanya kwa sababu niligundua inahitaji fedha, siyo nyingi sana, lakini nilikuwa nimeshakatishwa tamaa na watu wengi walionizunguka,” anakumbuka Madam Rita. Hata hivyo, ongezeko la wasanii waliokuwa

 

na vipaji, lakini hawana uwezo na waliomsumbua awasaidie walizidi kumsukuma zaidi kulifanyia kazi wazo hilo.

“Tukawa tunafanya kazi zingine, tukafanya kazi moja ya Wizara ya Afya, wakatulipa pesa nzuri, nikasema ‘this time I am going to do Bongo Star Search.”

Mara ya kwanza alitamani kufanya Bongo Star Search Dar es Salaam peke yake. Anakumbuka kuwa kutokana na bajeti yake ndogo waliyokuwa nayo, walifanya matangazo kwa kiasi kidogo tu kuhusiana na usaili ambao ulifanyika katika klabu ya usiku ya Bilicanas.

“Nakumbuka mtu wa kwanza niliyetengeneza naye tangazo fupi la ku-promote Bongo Star Search alikuwa ni AY. Alikuwa mdogo sana, alikuwa hajawa staa mkubwa,” anasema Rita.

Anasema siku ya usaili aliamini kuwa mahudhurio yangekuwa machache mno, lakini kwa kuwa alikuwa ameyavulia maji ilimlazimu kuyaoga.

“Ni kama kila mtu alikuwa haamini idea yangu ya kuanzisha mashindano haya kwa sababu tulijaribu kutangaza kwenye magazeti kwa miaka mitatu kila mtu alikuwa anatuambia ‘tutawatafuta.’

“Tulisema watu wafike saa 12:00 jioni. Mimi nikatoka nyumbani naendesha gari, nimefika Bilicanas ilikuwa kama saa 11:30, karibu nipate ajali! Sikutegemea, watu walikuwa wamepanga mstari kutoka Bilicanas mpaka Ofisi za Posta Nikatamani nirudi nyumbani, ‘we can’t, tutaanzia wapi,” alisema Madam Rita anasema usaili huo ulifanyika kwa siku tatu na mtu wa kwanza kufika alikuwa ni Jumanne Idd aliyefika saa 10:00 alfajiri na ndiye alikuwa mshindi kwa mwaka huo wa 2007.

AMINI KATIKA NDOTO

Ninachotaka ujue, kwanza ni kuamini katika ndoto na pili kama ndoto itashindikana amini katika kile unachoona kitaweza kukuinua bila kukata tamaa. Madam Rita anasema katika ndoto zake alitamani sana siku moja kuwa mwanasheria kwa sababu ilikuwa ndoto yake, lakini katikati ya masomo yake ndoto ilikatishwa na kuwa mama akiwa na umri mdogo.

“Nikafikiria nakatisha vipi ndoto zangu za muda mrefu, kwa hiyo sikuwa mwanasheria na tena sikujuta na sitakuja kujuta. Nikawa napenda mambo ya drama, nakumbuka nikiwa Zimbabwe nilikuwa natokea hadi kwenye mashindano ya urembo, kutangaza viatu, dawa za meno na mengine mengi, kwa hiyo nikawa nimeingia rasmi huko kufanya mambo ya TV na nilipokuja Dar ndipo nikaendeleza wazo hilo kupitia kampuni yangu,” anasema Madam Rita.

Makala: Imelda Mtema

Comments are closed.