The House of Favourite Newspapers

MADEE AMCHANA MTU VIWEMBE, ASAKWA NAPOLISI

KATIKA toleo lililopita, Madee aliendelea kuelezea historia ya maisha yake, aliishia pale alipoona maisha ya Sauz siyo kitu, akarejea Bongo. Huku Bongo akakutana na misala kibao. Fuatilia simulizi hii ufahamu kwa kina.

 

“KAMA utakuwa unakumbuka vizuri hapo mwanzo nilisema wakati naandaa tamasha la kwanza la mamisi nilimfanya mchumba wangu anayeitwa Joah kuwa mshindi.

“Ila pia watu wanatakiwa kujua kuwa muda huo nampa Joah ushindi katika mashindano hayo, huyo ndiye alikuwa mchumba wangu wa kwanza katika maisha yangu.

 

“Joah alikuwa akisoma Manzese, baadaye alihamishiwa nchini Kenya katika shule moja ilikuwa ikiitwa Vika.

“Kwa ujumla kipindi hicho pamoja na kwamba mimi nilikuwa mdogo lakini nilikuwa katika makundi ya vuruguvurugu sana maana nakumbuka kulikuwa na mchizi wangu mmoja hivi kampani yao ilikuwa nyuma ya mtaa wetu tu pale nyumbani maana hao machizi walikuwa wakikutafuta bora utafutwe na polisi kwani walikuwa wakitupiga balaa kiasi kwamba hata nyumbani unaweza usitoke hata mwezi ukisikia wanakusaka.

 

“Kuna tukio huwa silisahau maana kuna siku moja enzi hizo za kuandaa matamasha mimi na wanangu tulikuwa tuna timu inaitwa Everton, mimi nilikuwa nacheza sana mpira hata kundi la hao wanangu liliunganishwa na mpira, sasa kuna kombe moja hivi la mbuzi lilianzishwa, siku ya kwanza tulienda kucheza tukashinda.

 

“Wakati mechi ya nusu fainali ilipowadia, sisi tukapita zetu mtaani na kuwachangisha michango wana karibia wote, walikuwa wakituamini sana, lakini kwa bahati mbaya tulipoenda kule tulifungwa, sasa wakati tunarudi tukiwa kwenye gari, tukaambizana tusiseme kama tumefungwa, hivyo tulipofika mtaani tukaanza kushangilia hivyo kila mmoja akajua tumetinga fainali kumbe siyo.

 

“Basi baada ya kufika siku ya fainali tulichangishana tena na watu walichanga karibia mitaa yote ya jirani ukiwemo na ule wa wana, sisi tukawa tumetafuta mechi ya kirafiki ila ikawa kama siri yetu tu, hivyo ilipofika jioni tukaenda zetu tukacheza tukawashinda wakati huo tukawa tumeandaa mbuzi kwa fedha zile za michango hivyo baada ya mechi yule mbuzi akaletwa na baadhi yetu tukampandisha katika gari baada ya kufika Manzese shangwe zikatawala kuwa tumetwaa kombe kumbe ilikuwa ni janja yetu tu.

 

“Baada ya hapo yule mbuzi akawa tu anashinda kwetu anazurura, hivyo siku moja serikali ya mtaa ikatangaza mbuzi hawatakiwi mtaani, sasa sisi hatukusikia tangazo lile, yule mbuzi akachukuliwa na manispaa baada ya kufuatilia tukaonyeshwa zile sheria basi hatukuweza kushindana na serikali, tukawa wapole, lakini wakati mbuzi amepotea kuna mwenzetu mmoja akavujisha siri kuwa hatukucheza fainali tulifungwa ila tukadanganya, si wale wana wakorofi wakasikia.

 

“Basi ulikuwa msala mtaani, walianza kutusaka, wakaanzisha fujo shuleni kwetu pale Mpakani, baadaye kidogo zile fujo zikapoa, tukaondoka zetu, kumbe wale jamaa hawakuishia hapo, baadaye usiku kama mida ya saa mbili hivi wakaja na gari, wakafika wakachaguachagua wale wakorofi nikiwemo na mimi wakaanza kutushushia kichapo, wakati huo mimi nilikuwa nimejiandaa kwa sababu nilisikia kwamba watarudi.

 

“Nilijiandaa nikiwa na wembe wangu, kuna mchizi mmoja anaitwa Saleh Kioko akaanza kunipiga ngumi maana yeye alikuwa anafanya sana mazoezi, wakati huo mimi nilikuwa fundi sana wa kupiga roba, yaani nikikupiga moja hiyo hauchomoki.

 

“Basi nikambana yule jamaa, nikaanza kumchana na viwembe, akapiga sana kelele, nilipomuachia nikaona damu zinamwagika, nikakimbilia Kinondoni, huku nyumbani nikaacha kesi kubwa, polisi wakaja kumkamata kaka yangu ili apelekwe mahakamani.”

Je, nini kilijiri, tukutane kwenye toleo lijalo Jumatatu ijayo.

CHAMPIONI JUMATATU | KILINGE: MUSA MATEJA

Comments are closed.