The House of Favourite Newspapers

Madhara Ya Kuwaachia Ndugu Waishikilie Ndoa Yako Yapo Hapa

UHUSIANO wiwote unajengwa na upendo, uaminifu na msamaha. Kila mtu anapaswa kumpenda mwenzake, kumthamini na kumjali. Hii haishii hapo, ukishampenda na kumthamini, unapaswa kuwa mwaminifu kwake.

Usipokuwa mwaminifu, maisha ya uhusiano hayawezi kuwa na uhai. Hakuna mtu anayeweza kufurahia kusalitiwa. Usaliti unauma hivyo ni vyema kila mtu akaepuka usaliti. Si mwanaume wala mwanamke, hakuna mwenye kibali cha usaliti.

Usaliti unaharibu uhusiano. Usaliti unabomoa ndoa. Wanandoa wanapaswa kutosaliti kabisa. Kama hiyo haitoshi, ili waweze kudumisha amani ndani ya nyumba, kila mmoja wao anapaswa kujua kusamehe.

Kila binadamu ana upungufu. Hakuna aliyekamilika hivyo inapotokea mmekwaruzana ndani ya nyumba, ni vyema mkaombana msamaha. Anayeomba msamaha, aombe kwa dhati na wewe unayeombwa, basi uwe tayari kusamehe kutoka moyoni.

Mkisameheana, mkachukuliana udhaifu, hakika hakuna kitakachowashinda. Kila mmoja abebe udhaifu wa mwenzake, aone kwamba hajakamilika na anahitaji kufanyia kazi udhaifu wake kwa muda fulani ili aweze kubadilika.

Marafiki zangu, maisha ya ndoa yanahitaji usiri. Kila mmoja wenu awe na kifua cha kuhifadhi mambo. Ndoa ni taasisi ambayo wenye haki miliki ya ndoa hiyo ni ninyi wawili. Kila mmoja kwa nafasi yake, ana wajibu wa kutimiza majukumu yake ili muweze kufika salama.

Asiwepo hata mmoja wa kumdharau mwenzake. Kila mmoja amuone mwenzake ana umuhimu katika kuhakikisha mnafikia kwenye hatua ya mafanikio ambayo ninyi wawili mtakuwa mmepanga kuifikia. Iwe ndani ya mwaka mmoja au miaka kadhaa.

Jamani kuna madhara makubwa sana katika ndoa endapo tu utaruhusu ndoa yako ishikiliwe na ndugu. Ndugu wanapaswa kuwa na nafasi yao katika familia yenu, lakini wawe na mipaka.

Kuna mambo ambayo mnatakiwa kuyashughulikia ninyi wenyewe.

Hata kama ni ushauri, inashauriwa uombe kwa wale waliokuzidi umri, lakini bado unaambiwa akili za kuambiwa changanya na zako. Sikiliza ushauri wa ndugu, lakini jukumu la kufanya uamuzi liwe la kwako.

Unapokuwa kila jambo unalipeleka kwa ndugu, unawapa nafasi kuwa waamuzi wa ndoa yenu.

Ndugu wanakuwa wanawajua vizuri kuliko hata mnavyojijua ninyi wenyewe, hilo ni tatizo. Mathalan mmegombana, kabla ya kufika kwa ndugu, hakikisheni mnalishughulikia ninyi wenyewe kwanza.

Msiwe wepesi wa kupeleka tatizo la ugomvi wenu kwa wazazi. Litatueni ninyi wenyewe kwa kufuata misingi ambayo mlifundishwa na wazazi wenu wakati kila mmoja alikuwa akiishi kwao.

Madhara ya kuwashirikisha ndugu hufika mahali wao ndiyo wanageuka wapangaji wa mambo yenu.

Watawapangia matumizi, watawapangia miradi mnayopaswa kuifanya na kuwataka muache miradi fulani kutokana na matakwa yao, hiyo ni hatari. Watawatoa kwenye mstari wenu ambao mnapaswa wenyewe kujiamulia.

Wanandoa ndiyo madereva wa ndoa. Ninyi ndiyo mnashauriana kwa hoja. Mke aweke hoja zake mezani, mume naye azisikilize na mwisho wa siku muwe na jibu la pamoja. Mume naye aje na hoja zake, mke azisikilize, ashauri na kuboresha na mwisho wa siku mnaamua kwa pamoja.

Jambo mtakaloamua ninyi wawili, ndilo litakuwa dira yenu. Ndilo litakalokuwa kama katiba au sheria ya maisha yenu. Asiwepo mtu wa kuwakosoa au kuwataka muishi kama fulani anavyoishi. Ninyi mbaki kuwa ninyi na kama mtapatia, watakuja kuwapongeza baadaye.

Hata ikitokea mmekosea, msikate tamaa. Hayo ni maisha yenu na kama bado mnapumua, mna nafasi nyingine ya kuboresha safari yenu. Mnaruhusiwa kujifunza mazuri kupitia wenzenu, lakini lazima mchuje, mlitafakari kwa pamoja na kutoka na jibu lenu.

Mtakaloamua ndilo lenu. Ukiruhusu sana ndugu waingilie ndoa yenu, wanaweza hata kuwashauri muachane maana wao hawajui thamani ya penzi lenu. Ni rahisi tu kuwaambia; ‘achana naye bwana.’

 

Comments are closed.