The House of Favourite Newspapers

Mahakama Yamgomea Kabendera Kumzika Mama Yake – Video

0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemnyima kibali mwandishi wa habari, Erick Kabendera, kwenda kushiriki ibada ya maziko ya mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi.

 

Hiyo imebainika leo katika mahakama hiyo wakati Kabendera anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha alipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kesi yake kutajwa.

 

Katika mwendelezo huo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon,  amemueleza Hakimu Mkazi, Janeth Mtega,  kwamba jamhuri inampa pole Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi.

 

Hata hivyo, Hakimu Mtega ameiahirisha kesi hiyo hadi saa 8:45 mchana (lo) kwa ajili ya kutoa uamuzi kama Kabendera ashiriki maziko hayo au la.

 

Wakili Wankyo amedai kuwa maombi ya Kabendera kupitia mawakili wake yamewasilishwa wakati ambao si sahihi kwa sababu mahakama haina mamlaka na pia Mkurugenzi wa Mashitaka hajaipa kibali ya kusikiliza kesi hiyo.

 

Kukataliwa kwa Kabendera kushiriki mazishi ya mama yake, kumeibuka kutokana na maombi aliyoyatoa Kabendera kupitia mawakili wake akiwemo Jebra Kambole.

 

Wakili Kambole amedai wanaiomba mahakama hiyo imruhusu Kabendera akashiriki maziko ya mama yake mzazi katika Kanisa la Roman Katoliki lilipo Chang’ombe majira ya mchana.

 

Kambole ameieleza mahakama kuwa suala la kushiriki sala ya mwisho ya msiba ni haki ya binadamu na suala la faragha.

 

“Kushindwa kuhudhuria maziko ya mama yake tutakuwa tumemuadhibu adhabu kubwa tena kwa kuangalia uhusiano wa mshitakiwa na mama yake mzazi kwani alikuwa akimuuguza na ni vizuri akatoa heshima ya mwisho,”ameeleza.

 

Wakili Jebra amedai kuwa ni muhimu kwa Kabendera kushiriki kwa sababu mama mzazi ni mmoja, akifa anaagwa mara moja.

 

 

Mama Kabendera alifariki dunia Desemba 31, 2019,  ikiwa ni wiki kadhaa baada ya kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amsamehe mwanaye huyo,.

 

Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la utakatishaji wa Sh.Mil 173.

Leave A Reply