The House of Favourite Newspapers

Mahakama Yakataa Ombi la Kukamatwa Shahidi Kesi ya Sabaya

0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali ombi la kutoa hati ya kukamatwa shahidi wa 10 wa Jamhuri, Francis Mroso baada ya ombi hilo kutokidhi matakwa ya kisheria.

 

Desemba 1, 2921 Wakili wa utetezi Fridolin Bwemelo aliomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwa shahidi huyo akidai alitoa rushwa ya Tsh 90 milioni.

 

Mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, Wakili Bwemelo aliiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa shahidi huyo kaani alikiri kutoa rushwa hiyo.

 

Jana Desemba 6, 2021 upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Ofmed Mtenga, Felix Kwetukia na Wakili wa Serikali Neema Mbwana huku utetezi ukiwakilishwa na Wakili Bwemelo aliyekuwa anawashikia mikoba mawakili wenzake.

 

Akitoa uamuzi huo mdogo, Hakimu huyo alisema mahakama inatupilia mbali ombi hilo kwani halijakidhi matakwa ya Sheria inayoruhusu mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa shahidi huyo.

Alisema kifungu namba 52(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kinamlinda shahidi anapotoa ushahidi akiwa chini ya kiapo.

 

“Ombi la Wakili wa utetezi halijakidhi matakwa ya Sheria inayoruhusu mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa shahidi na mahakama imetupilia mbali maombi na inaona iendelee kusikiliza shahidi anayefuata,” alisema

“Kifungu cha 52(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kinamlinda shahidi anapotoa ushahidi wake mahakamani akiwa chini ya kiapo,” alisema hakimu.

 

Baada ya uamuzi huo mdogo Wakili Mtenga aliomba mahakama iahirishe shauri hilo hadi leo Desemba 7, kwa ajili ya kuendelea na shahidi wa 11 wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi, ombi ambalo halikupingwa na wakili Bwemelo.

 

Awali Desemba 2, wakiwasilisha hoja juu ya ombi hilo, Wakili Kwetukia,aliiomba mahakama kutupilia mbali ombi hilo, kwani liko nje ya muktadha wa kisheria.

Mbali na Sabaya, watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

 

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano, la kwanza wakidaiwa Januari 22 mwaka huu ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

 

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Leave A Reply