The House of Favourite Newspapers

Mtuhumiwa wa Mauaji ya Mwangosi Akutwa na Kesi ya Kujibu

0

Mwangosi

Daud Mwangosi enzi za uhai wake.

Na  Francis Godwin, Iringa

KESI ya mauaji ya aliyekuwa  mwandishi  wa habari wa Channel Ten na Mwenyekiti  wa Chama cha waandishi wa  Habari Mkoa  wa  Iringa, Daud Mwangosi imeendelea kusikilizwa huku Mahakama Kuu Kanda ya Iringa  ikisema  kuwa mtuhumiwa wa kesi ya mauaji hayo Pacificius Cleophace Simon ana kesi  ya  kujibu.

Akitoa uamuzi huo leo, Jaji wa mahakama hiyo, Paul Kiwelo amesema; “Mahakama imejiridhisha kwamba katika shauri lililoko mbele yetu, tuhuma ambazo zimetolewa dhidi ya mtuhumiwa na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri, mtuhumiwa ana kesi ya kujibu kwa hiyo natupilia mbali ombi la upande wa utetezi lililotaka kesi hii itupiliwe mbali kwa madai kwamba hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaomuhusisha mtuhumiwa na mauaji hayo.”

Jaji Kiwelo alisema mtuhumiwa huyo ataanza kujitetea kesho baada ya kuridhia ombi hilo lililotolewa na wakili wa upande wa utetezi Rwezaula Kaijage na kuungwa mkono na mawakili wa Jamuhuri, Sandy Hyra na Ladslaus Komanya.

Mara baada ya Jaji huyo kutoa uamuzi huo, askari polisi zaidi ya 20 waliokuwa ndani ya chumba cha mahakama hiyo, walimfunika shuka mtuhumiwa huyo ili wanahabari wasipate fursa ya kumpiga picha.

Mtuhumiwa huyo alitolewa mahakamani hapo na kundi la askari hao, akiwa amefichwa katikati yao, hatua ambayo pia iliwazuia wanahabari kufanya kazi yao vizuri.

Tofauti na watuhumiwa wengine, mtuhumiwa huyo aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Iringa aliondolewa katika eneo la mahakama kwa kutumia gari dogo la polisi aina ya Land Rover badala ya kupandishwa katika kalandinga kama inavyofanywa kwa watuhumiwa wengine.

Mtuhumiwa  huyo anatuhumiwa  kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012.

mwangosi 2

Mwangosi kabla ya kuuawa.

Leave A Reply