The House of Favourite Newspapers

MAISHA MAPYA YA JOKATE USIPIME!

MKUU

DAR ES SALAAM: Maisha mapya ya mwanamitindo Jokate Mwegelo yametajwa kuwa ya tofauti na huenda yakampa taabu sana mrembo huyo ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

MAISHA MAPYA YATAKUWAJE?

Gazeti hili lilifunga safari na kufika nyumbani kwake ambako lilikuta wafanyakazi kadhaa waliokuwa wakiifanyia usafi tayari kwa ajili ya kuhamia mrembo huyo. Kwa nyakati tofauti, wafanyakazi hao walieleza kufurahishwa na uteuzi huo wa binti waliyemwita mdogo kiumri na kwa kutumia uzoefu wao, wakaeleza namna uteuzi huo utakavyomlazimu kubadili mfumo wa maisha.

Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema Jokate atalazimika kubadilika sana. “Naamini mwanzoni lazima atapata taabu kuji-adjust kulingana na maisha yake ya sasa. Maana sasa ni kiongozi wa umma na viongozi wa umma wana maadili yao ambayo ni tofauti na wanamitindo au mastaa,” alisema.

RATIBA YA SIKU KUBADILIKA

Mfanyakazi mwingine alisema ratiba ya kazi na majukumu mapya ya Ukuu wa Wilaya yatamlazimisha kuondokana na ratiba ya zamani, ikiwemo kuacha kuwa mwanamitindo na usanii kwani baadhi ya mambo hawezi kufanya akiwa kiongozi wa umma.

“Hapa kila kitu kinaratibiwa, atakuwa na muda mfupi sana kufanya mambo yake binafsi maana sisi tuliona hata kwa mkuu wa wilaya aliyepita. Kila kitu ni ratiba, kuna muda wa kutoka, kuna muda wa kurudi kwa wiki nzima.

“Fikiria kwamba lazima atakuwa na gari na dereva wake ambaye lazima atakuwa naye popote anapoenda. Pia hapa nyumbani kunakuwa na ulinzi mkali wa askari polisi wa kuzuia fujo, saa ngapi ataendeleza uanamitindo?” alihoji.

KUWAPOTEZA MARAFIKI

Mbali na ratiba, mfanyakazi huyo alisema kitendo tu cha kubadili mazingira kutoka kuishi na wazazi wake hadi maisha ya kujitegemea, kitamlazimu abadili mtazamo wa maisha. “Kuna baadhi ya marafiki atawapoteza kwa sababu hawatakuwa na fursa ya kukutana naye wakati wanaotaka wao, mambo ya muziki na kujirusha pia lazima yakae pembeni,” alisema na kusisitiza.

Mfanyakazi huyo aliongeza kuwa, mbali na dereva atakayemuendesha katika gari lake la kifahari aina ya Land Cruiser Prado Tx linalotajwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 90, Jokate huenda akawa sasa na msaidizi maalum ambaye itamlazimu hata simu za wale mashoga zake kupokelewa na kuchujwa na msaidizi huyo.

“Yaani zile simu za mambo ya hovyo ambazo wasanii wenzake walikuwa wamezoea tu kupiga wakati wowote iwe usiku au mchana zitachujwa kwa sasa,” alisema.

OFISINI ATABANWA MNO

Mbali na maisha ya nyumbani, Risasi Mchanganyiko lilifika pia ofisini kwake na kuelezwa kuwa, ratiba pia itambana mno kwani mbali na kazi za ofisini atakuwa na ratiba kibao za kushughulikia kero mbalimbali za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi.

AFUTA PICHA ZA ZAMANI

Wakati wafanyakazi hao wakieleza maisha mapya ya DC huyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, Jokate alifuta picha zake zote kwenye mtandao wa Instagram tukio linalotafsiriwa na wengi kuwa ndiyo sehemu ya maisha hayo mapya ya ukuu wa wilaya.

MWENYEWE ANASEMAJE?

Hata hivyo, hivi karibuni Jokate alikaririwa akieleza kuwa ingawa atalazimika kubadilika kidogo, ataendelea kuwaunga mkono wanamitindo na yeye hataacha kuwa mwanamitindo kama baadhi ya watu wanavyodhani.

“Jamani mimi bado mrembo sitaacha kuwa mwanamitindo, nitavaa vitenge na nguo mbalimbali za wabunifu wa ndani, ila kwa sasa lazima kuwe na utaratibu wa mavazi lazima nibadilike kidogo, nivae kama mtumishi wa umma,” alisema na kuendelea; “Ikumbukwe kuna mitindo ya mafuta, wanja nao ni urembo lazima tuendelee nao kwa sababu haya ni maisha ya kila siku, nitaendelea kusapoti mitindo na huuhuu ukuu wa wilaya wangu,” alisema.

TUJIKUMBUSHE

Julai 29, mwaka huu, Rais Dk John Magufuli alifanya uteuzi wa makatibu tawala, wakuu wa mikoa na wilaya makatibu wakuu na manaibu wao, huku Jokate akimpangia nafasi hiyo ya ukuu wa wilaya.

Jokate aliyeshika nafasi ya pili katika Shindano la Miss Tanzania mwaka 2006, ameteuliwa katika nafasi hiyo siku kadhaa baada ya kuondolewa katika nafasi ya Kaimu Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Ikumbukwe kuwa Jokate pia alishawahi kueleza kuwa hatamani kuondoka nyumbani kwa wazazi wake mpaka atakapo-olewa, hivyo uteuzi huo pia unaweza ukawa umevuruga au kuboresha baadhi ya ndoto zake.

STORI: Richard Bukos, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.