The House of Favourite Newspapers

MAJALIWA: SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA UNHCR

Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa,  akiwa katika mzungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Filippo Grandi. Mazungumzo hayo yamefanyika sambamba na mkutano wa TICAD7 Yokohoma, Japan.

 

SERIKALI ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika kutatua changamoto zinazotokana na uwepo wa wakimbizi nchini  na kutafuta suluhu ya kudumu kwenye nchi zao ili wakimbizi hao waweze kurejea makwao kuendelea na shughuli za maendeleo.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Agosti 30, 2019) katika mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, kwenye Kituo cha Maonyesho cha Yokohama nchini Japan baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akifuatilia mazungumzo kati ya Majaliwa na  Grandi (hayupo pichani).

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa UNHCR kuisaidia mikoa inayokaliwa na wakimbizi kutokana na kuharibiwa kwa mazingira.

“Hata hivyo,  Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na UNHCR kuimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na utulivu,” alisema.

Naye Grandi amesema amefurahishwa na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kupokea wakimbizi na usikivu wa Rais  John Magufuli katika kushughulikia changamoto za wakimbizi.

Majaliwa yupo Japan akimwakilisha Rais  Magufuli kwenye TICAD 7 ambao umehitimishwa leo akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Muungano  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Majaliwa akiagana  na Grandi baada ya mazungumzo.

Comments are closed.