The House of Favourite Newspapers

Majambazi wawili wauawa katika majibizano na polisi wilayani Rungwe

kamanda-KidavashariMBEYA: Watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na bunduki tatu zimekatwa kwenye mapambano ya kujibizana risasi baina ya askari wa jeshi la polisi na majambazi katika kijiji cha Busisya, kata ya Kisiba wilayani Rungwe, wakati watu hao wakiwa njiani kuelekea katika kata ya Mbambo kwa lengo la kupora katika duka la mfanyabiashara mmoja anayeuza bia za jumla.

Kamanda wa polisi mkoa wa mbeya, Naibu Kamishna wa jeshi la polisi Dhahir Athuman Kidavashari amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 1:45 usiku katika kijiji cha Busisya kwenye barabara ya Tukuyu – Mbambo, ikiwa ni baada ya Jeshi la polisi kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema juu ya uwepo wa watu waliopanga kwenda kuvamia duka la mfanyabiashara bia za jumla katika kijiji cha Mbambo.

Kamanda Kidavashari amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, polisi wakaweka mtego njiani katika kijiji cha Busisya na ndipo watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa wamebebana watatu kwenye pikipiki moja wakajitokeza na waliposimamishwa na askari wakaanza kurusha risasi, hali ambayo ikawalazimu polisi kujibu mapigo na kuwaua wawili papo hapo huku mmoja akifanikiwa kukimbia na pikipiki.

Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, baada ya watu hao kuuawa, miili yao imepekuliwa na kukutwa bunduki tatu ambazo ni bunduki aina ya Mark IV yenye namba 38482, Short Gun greener yenye namba G73878 kila moja ikiwa na risasi mbili huku zikiwa zimekatwa vitako kurahisisha ubebaji pamoja na gobore lililotengenezwa kienyeji lakini lenye uwezo wa kutumia risasi za bunduki ya short gun na lenyewe likiwa na risasi sita huku pia watu hao wakiwa na zana nyingine kama mavazi, begi na bisibisi.

Kamanda Kidavashari amesema miili ya watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi bado haijatambulika na hivi sasa imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Rungwe ya Makandana ambapo ametoa wito kwa watu kufika hospitalini hapo kuitambua.

Katika tukio lingine Kamanda Kidavashari amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori wamefanya msako wilayani chunya na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja akiwa na meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilogramu 61.

Chanzo: ITV

Comments are closed.