The House of Favourite Newspapers

Majembe Manne Yabadili Vikosi Simba, Yanga

0
Kikosi cha Simba.

USAJILI wa dirisha dogo kwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, unaendelea tangu ulipofunguliwa Novemba 15, mwaka huu. Zimebaki siku chache sana kuanzia leo kabla ya dirisha hilo halijafungwa Desemba 15, mwaka huu. Wakati zoezi hilo likiendelea, tayari Yanga imeshatangaza kuwasajili nyota wawili, Fiston Kayembe raia wa DR Congo na kinda wa Kitanzania, Yohana Nkomola.

 

Kwa upande wa Simba, bado haijasajili, lakini kuna baadhi ya wachezaji wanatajwa kutakiwa kikosini hapo na ambao wanaonekana wakiingia ni wazi watabadilisha sura ya kikosi hicho kama ilivyo kwa Yanga. Makala haya, inakuchambulia nyota hao ambao ilikuwa lazima wasajiliwe kipindi hiki na kubadilisha vikosi vya timu hasa Simba na Yanga ambazo zitaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa hapo mwakani.

Kikosi cha Yanga.

Fiston Kayembe- Yanga

Beki huyo anatajwa kuwa ni mmoja kati ya walinzi ambao wana uwezo wa hali ya juu katika kupambana na huenda akaibeba Yanga hasa katika michuano ya kimataifa.

Ujio wake ndani ya Yanga, unatazamiwa kuwa tofauti hasa katika safu ya ulinzi ambapo ilionekana kuwa na mapungufu kidogo baada ya kuondoka kwa Vincent Bossou raia wa Togo.

 

Kayembe kabla ya kupewa mkataba wa miaka miwili, alifanya majaribio na timu hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu, lakini wakati akifanya majaribio hayo, Yanga ilianza harakati za kumrudisha Bossou, ikashindikana.

Kayembe anaungana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ katika nafasi ya ulinzi wa beki wa kati jambo ambalo linatoa wigo mpana katika safu hiyo kuelekea kwenye michuano ya Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi za kumalizia Ligi Kuu Bara, kuna dalili kuwa atakuwa kwenye kikosi cha kwanza.

Yohana Nkomola- Yanga

Hili ni moja kati ya mazao ya timu za vijana ya Serengeti Boys. Amesajiliwa Yanga baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia, George Lwandamina kuweza kuvutiwa na kiwango chake. Huyu ni kinda ambaye anaenda kuingia katika kikosi cha mabingwa wa tetezi wa Ligi Kuu Bara, ujio wake ndani ya Yanga, haumaanishi mara moja atakibadilisha kikosi hicho, bali ataongeza nguvu na kukifanya kikosi hicho kuwa kipana zaidi.

Asante Kwasi -Simba

BEKI kisiki na tegemeo ndani ya kikosi cha Lipuli FC ya Iringa. Anatajwa kutakiwa na Simba ambayo ilianza kumfuatilia tangu dirisha kubwa la usajili msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake ndani ya Mbao FC.

Kwasi ambaye kwa sasa ndiye kinara wa ufungaji katika timu yake akiwa na mabao manne, anatakiwa na Simba kuchukua nafasi ya Method Mwanjale na Juuko Murshid. Mwanjale ambaye amekuwa majeruhi mara kwa mara, anatafutiwa mbadala wake ambaye ni Kwasi, lakini pia hata Juuko yupo mbioni kuondoka kikosini hapo, hivyo beki huyo wa kimataifa kutoka Ghana ni chaguo la kwanza la Kocha wa Simba, Joseph Omog.

 

Ismaila Diara – Simba

Simba licha ya kuwa na watu wengi kwenye safu yake ya ushambuliaji, lakini inahitaji straika mwingine wa kuleta changamoto mpya baada ya kuonekana Emmanuel Okwi kuwa tegemeo zaidi ya wengine.

 

 

Okwi, John Bocco, Laudit Mavugo, Juma Liuzio na Nicholaus Gyan, ndiyo wanaoongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo wakisaidiwa na Shiza Kichuya anayechezea nafasi ya kiungo mshambuliaji. Ukimuondoa Bocco na Okwi, waliobaki kwenye nafasi ya ushambuliaji, wameonekana hawawezi kuibeba timu hiyo na ndiyo maana Mavugo na Liuzio wanatajwa kutaka kuondoka kikosini hapo kumpisha Ismail Diara raia wa Mali anayeichezea Rayon Sports ya Rwanda.

 

Diara inaripotiwa kwamba, ameshafanya mazungumzo ya awali na Simba, kilichopo sasa ni makubaliano ya Klabu ya Simba na Rayon, kisha ndiyo uamuzi utoke juu ya mchezaji huyo atakuwa wapi. Diara sifa zake, kwanza ni msumbufu kwa mabeki, anajituma na haogopi kupambana na beki wa aina yoyote yule, hivyo akijiunga na timu hiyo, atasaidia sana kwenye idara hiyo na kuifanya Simba kuwa na makali zaidi.

STORI: MARTHA MBOMA NA OMARY MDOSE.

Matukio kama haya na mengine, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

VIDEO: DK SHIKA KUWEKA HISTORIA USIKU WA 900 ITAPENDEZA

Leave A Reply