The House of Favourite Newspapers

MAJI YENYE SUMU YAZUA BALAA!

Maji yanayodaiwa kuwa na kemikali zenye sumu yanayotoka kwenye kiwanda kimoja cha sabuni kilichopo maeneo ya Vingunguti, Barabara ya Tazara jijini Dar yamezua balaa kubwa kwa kuwaathiri watu wengi.

 

Awali, gazeti hili lilipokea simu kutoka kwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo akieleza kuwa, maji hayo yanayotiririka kutoka kwenye kiwanda hicho yamemuathiri vibaya mwanafunzi wa Sekondari ya Kivule aliyefahamika kwa jina la Ramadhan Athuman huku wengine wakiugulia majumbani kwao.

 

“Jamani hebu njooni muone tunavyomalizwa, kuna kiwanda kimoja kipo mitaa yetu, sasa maji yenye sumu yanayotoka huko yanaletea madhara makubwa. Nina ndugu yangu hapa miguu imebabuka kwa sababu ya kupita kwenye maji hayo,” alidai mtoa habari huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sakina.

Baada ya kupata taarifa hizo, mwandishi wetu alifika hadi eneo hilo na kufanikiwa kumuona mwanafunzi huyo aliyeathirika vibaya miguu baada ya kupita kwenye maji hayo.

 

Akizungumza na Risasi, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Sada Omari alisema kuwa, anakumbuka siku chache baada ya mvua kuanza kuna siku mvua kubwa ilinyesha na barabara wanayopita kujaa maji (Barabara ya Tazara) ambapo mwanaye hupita akienda shule.

“Nakumbuka siku mwanangu alipopita alikuja na kusema alisikia anawashwa sana mwilini sehemu ya miguu lakini hakujali kwani wengi wamekuwa wakipita na kuwashwa lakini baadaye hali hiyo huwa inaisha,” alisema mama huyo.

 

 Aidha alisema kuwa, mwanaye aliposikia anawashwa aliendelea na safari yake ya kwenda shule lakini alipofika huko hali ilibadilika, akaugua homa ghafla na kuvimba miguu ambayo ilianza kutokwa na malengelenge na baadaye kubabuka.

“Baada ya kupatwa na hali ya homa na miguu kubabuka kama mtu aliyeungua, alirudishwa nyumbani tukaenda Hospitali ya Amana ambapo alipimwa na kugundulika amepita kwenye maji yenye sumu,” alidai mama huyo.

 

Akizungumza na mwandishi wetu, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Faru, Simba Said Simba ambaye wakazi wake hupita kwenye maji hayo alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa watu wengi kuhusiana na madhara wanayopata kutokana na maji hayo.

“Nina malalamiko ya zaidi ya watu kumi ambao wote wamebabuka kwa sababu ya maji hayo, hili tatizo nimeshalipeleka kwenye ngazi ya manispaa kwani ni tatizo kubwa ambalo linawagusa wapita njia wengi,” alisema mwenyekiti huyo.

 

Mwandishi wetu pia alifika kwenye kiwanda ambacho kinalalamikiwa kutiririsha maji hayo lakini alikutana na wafanyakazi waliosema wao si waongeaji na kuagiza watafutwe wasemaji wa kiwanda.

Na Hamida Hassan, Risasi Jumamosi.

Comments are closed.