The House of Favourite Newspapers

Makaburi Ajali ya Mafuta Moro, Yajengewa Ukuta

HATIMAYE ujenzi wa ukuta unaozunguka makaburi ya watu waliofariki kwenye ajali ya mlipuko wa lori la mafuta umeanza.

 

Hivi karibuni,  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,  alikaririwa akipinga gharama ya shilingi milioni 30 ya kujenga ukuta huo iliyopendekezwa na wahusika wa kazi hiyo.

”Eneo lile la makaburi ni nusu heka hivyo kiasi hicho cha milioni 30 ni kikubwa mno sisi kama serikali tutatoa milioni 10 kwa ujenzi wa ukuta huo,” alikaririwa akisema  Majaliwa akisema alipofanya ziara mkoani hapa.

 

Kufuatia hali hiyo, mwandishi wa mtandao huu aliamua kutinga kwenye makaburi hayo yaliyopo Kolla kwa lengo la kuchunguza kama ujenzi huo umeanza au la.

Ingawa hakukuta mafundi lakini alishuhudia kazi ya ujenzi wa ukuta huo ukianza kwa hatua za kuchimba msingi wa kiwango kizuri kuzunguka eneo lote la makaburi hayo sambamba na kushuhudia malundo ya mchanga, kokoto na matofali yakiwa eneo la ujenzi. 

 

Kwa kuwa hakuwepo mtu yoyote eneo hilo mtandao huu ulishindwa kubaini wasimamizi wa ujenzi huo pamoja na kampuni iliyopewa tenda ya kujenga ukuta huo.  Hata hivyo, juhudi za mtandao huu kuwatafuta wahusika hao ili wazungumzie ujenzi huo zinaendelea.

TUJIKUMBUSHE
Agosti 10 mwaka huu lori lililobeba mafuta ya petroli likitokea Dar es Salaam kuelekea lringa lilipinduka eneo la Msamvu-Itigi mjini Morogoro na wananachi walijitokeza kwa wingi kuchukua mafuta yaliyokuwa katika gari hilo ambapo ilidaiwa katika harakati za kuchomoa betri ya gari hilo, mlipuko mkubwa ulitokea na kusababisha vifo vya watu 104, waliofia hapohapo na wengine mahospitalini.

Kundi kubwa la marehemu hao walizikwa eneo hilo la makaburi ya Kolla huku baadhi waliotambuliwa na ndugu zao wakienda kuzikwa nyumbani na kwenye mikoa yao.

Majaliwa, aliyemwalikisha Rais John P Magufuli kwenye mazishi hayo,  aliagiza ujengwe ukuta kuzunguka makaburi hayo.

Na Dunstan Shekidele | GPL, Morogoro.

Comments are closed.