The House of Favourite Newspapers

Makocha Simba Sh 320,000 Kwa Siku

ASIKWAMBIE mtu, Simba hivi sasa ipo vizuri kiuchumi. Katika kuthibitisha hilo uongozi wa klabu hiyo umewaandalia nyumba za kifahari makocha wake wapya, kocha mkuu wa timu, Mbelgiji, Patrick Aussems pamoja na kocha wa viungo, Mtunisia, Adel Zrane ambao kwa sasa wapo na kikosi cha timu hiyo nchini Uturuki.

 

Makocha hao wameandaliwa nyumba katika moja ya hoteli za hadhi ya juu jijini Dar es Salaam ambapo watakuwa wakiishi kwa kipindi chote watakachokuwa wakiifundisha timu hiyo.

 

Taarifa zilizofika katika gazeti hili inadaiwa kuwa gharama za nyumba hizo kwa siku moja ni Sh 160,000, hivyo kwa kuwa watakuwa wawili kila mmoja atalipiwa kiasi hicho na jumla kwa siku itakuwa ni Sh 320,000.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Ijumaa limezipata, zimeeleza kuwa uongozi huo umeamua kuwaweka makocha hao katika hoteli hiyo iliyo karibu kabisa na bahari kutokana na kuwa na mazingira ya tulivu.

“Kwa sasa makocha hao watakuwa wakiisha katika hoteli hiyo ambayo uongozi umewatafutia kutokana na kuvutiwa na mandhari yake ya utulivu lakini pia ubora wake.

 

“Hata hivyo, kabla ya timu kwenda Uturuki, Kocha Aussems alifika hotelini hapo na kuangalia chumba atakachokuwa akiisha na kuvutiwa nacho,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Gazeti hili linafahamu kuwa inapotokea kuna mteja wa muda mrefu hotelini ni rahisi kupunguziwa bei, hivyo kuna uwezekano na makocha hao wakapunguziwa bei ikiwa watadumu muda mrefu katika makazi hayo.

 

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Simba walipoulizwa kuhusiana na hilo hawakuwa tayari kusema chochote na kudai kuwa anayeweza kulizungumzia hilo ni kaimu rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’, lakini alipotafutwa hakupatikana.

Habari na Sweetbert Lukonge, Championi Ijumaa

Comments are closed.