The House of Favourite Newspapers

MAKONDA KUSOMESHA WANAFUNZI WA KIKE 100 – VIDEO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kike 100 ambao wamehitimu kidato cha nne na kufaulu kuendelea na masomo ya juu katika elimu ya kidato cha tano na sita.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 20, 2019, Makonda amesema ameanzisha mfuko maalum wa kuwasaidia watoto wa kike waliofaulu na ambao wamesoma katika mazingira magumu kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Aidha, Makonda amesema ufadhili huo utawahusu wanafunzi wa kike waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi na kuhakikisha wanafika elimu ya juu ili waweze kulisaidia taifa katika nyanja ya sayansi na teknolojia.

 

“Mimi nimeona nimuunge mkono Rais na katika namna ya kipekee nimeamua kutoa scholarship kwa watoto wakike 100 wanaomaliza masomo yao ya form four na kufaulu kupitia masomo ya Sayansi kuanzia mwaka huu katika Mkoa wa Dar, nitawasomesha kwa gharama zote za elimu kuanzia ada, vitabu, uniform, mabegi mpaka na pocket money kwa muda wao wote wa masomo mpaka kumaliza form five na Six,” amesema RC Makonda.

 

Amebainisha makundi ya watoto watakaonufaika na mfuko huo kuwa ni pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu lakini wamefanikiwa kufaulu, watoto yatima  na watoto wanaolelewa na mama wanaojihusisha na biashara ndogondogo.

 

Mfuko huo unaanza rasmi kufanya kazi mwaka huu ambapo kwa awamu ya kwanza utahusisha wanafunzi wa kike 100 waliofaulu kidato cha nne na kupata nafasi ya kuendelea kidato cha tano na sita.

 VIDEO: FUATILIA TUKIO HILO

Comments are closed.