The House of Favourite Newspapers

MAKONDA: WANAOTUMIA WATOTO YATIMA, WALEMAVU KAMA KITEGA UCHUMI KUKIONA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa  uzinduzi huo wa ripoti ya matokeo ya utafiti wa idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kinyume na sheria.

 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza vita na watu wenye tabia za kuwachukua watoto yatima, walemavu na waishio katika maisha magumu kama mitaji ya kujinufaisha watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

 

 

Makonda ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya matokeo ya utafiti wa idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kinyume na sheria hali inayopelekea kushindwa kutumia fursa ya elimu bure iliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli jambo ambalo Makonda ameapa kulivalia njuga.

Utafiti huo umebaini kwamba Mkoa wa Dar es Salaam pekee una jumla ya watoto 3,312 wanafanya kazi mitaani na kati ya hao watoto 2,984 walionekana wakifanya kazi nyakati za mchana na 328 wanafanya kazi nyakati za usiku.

 

 

Makonda amesema idadi hiyo ya watoto wanaoishi mitaani ni matokeo ya kukosekana kwa misingi bora ya familia na mmonyoko wa maadili ndiyo maana aliamua kuunda tume ya kupitia sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa ambayo itasaidia kuweka haki stahiki za watoto.

 

Aidha Makonda amewaonya watu wenye tabia ya kuwapatia ombaomba fedha barabarani kuwa ndiyo wanaohalalisha uwepo wa watu hao ambapo amesema kama mtu anataka kweli kusaidia waishio maisha magumu apeleke misaada hiyo kwenye vituo vilivyopo kwa mujibu wa sheria kwakuwa vituo hivyo vinafuatilia mienendo ya watoto kitabia, elimu na matibabu.

“Ukimpa pesa mtoto barabarani unatengeneza mazingira ya kuwa na fedha ambayo hana uhalali nayo na anapokuwa mtu mzima anakuwa mkabaji, mporaji na kuchoma visu watu wasio na hatia,” amesema Makonda.

 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Babawatoto Centre, Mgunga Mnyenyelwa, amempongeza Makonda kwa kufanya zoezi la kutafuta haki ya mtoto alietelekezwa kwakuwa kupitia zoezi hilo limewezesha watoto wengi kuingia kwenye mfumo rasmi wa kupata fedha ya matunzo kila mwezi pamoja na bima ya matibabu bure.

 

 

Amefafanua kuwa utafiti huo umefanywa na Shirika la Babawatoto Centre for Children And Youth kupitia mradi wa USAID Kizazi Kipya kwenye mikoa mitano ambapo wamebaini nusu ya watoto wa mitaani wanapatikana mkoa wa Dar es Salaam.

 

Comments are closed.