Mama Akutwa Mtupu Live, Azua Taharuki

MWANAMKE mmoja ambaye hakufahamika mara moja, amezua taharuki baada ya kukutwa mtupu kama alivyozaliwa eneo la Shani Sinema jirani na Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro.
Tukio hilo lililojaza watu sehemu hiyo lilijiri alfajiri ya Jumamosi iliyopita.

 

Mashuhuda wa tukio hilo wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara wa Mtaa wa Kitope unaoelekea Kituo Kikuu cha Polisi na wauza magazeti ‘mavenda’ waliokuwa wakienda kugawiwa magazeti kwenye Jengo la Shani Sinema.

 

Mwandishi wetu ambaye alimshuhudia mama huyo akiwa amezungukwa mtupu baada ya kuitwa eneo la tukio aliambiwa na mmoja wa wauza magazeti, Bwende Ally kuwa mama huyo alikutwa akiwa hivyo na kupigwa butwaa. Baadaye wasamaria wema waliokuwa eneo hilo walijitolea nguo aina ya khanga na fulana na kumvisha mama huyo.

 

Alipohojiwa na gazeti hili, mama huyo alikuwa na haya ya kusema:
“Jana usiku nilikuwa na wenzangu, tulitokea Kauzeni (jirani na Kambi ya Jeshi ya Mzinga) tukitumia usafiri wa ungo.

 

“Tulipofika eneo hili mimi nilianguka, wenzangu wakaendelea na safari.”
Baadaye walikuja Polisi watatu eneo la tukio, mmoja akiwa na sare za jeshi hilo huku wawili wakiwa wamevaa kiraia na wakamhoji.

 

Hata hivyo, Polisi hao walikataa kupigwa picha na wakaamua kuondoka eneo hilo huku wakisema hawahitaji kupigwa picha, jambo lililowashangaza wananchi waliofurika eneo hilo.

 

Baada ya Polisi hao kuondoka, baadhi ya wananchi walishauri wampeleke mama huyo kanisani au msikitini ili akaombewe ili aachane na mambo hayo ya kishirikina kama alivyodai na wengine wakidai maadam sasa amevaa nguo, aachwe aende anakokujua. Hadi mwandishi wetu anaondoka eneo la tukio, wananchi hao walikuwa wakivutana kila upande ukitetea hoja yake.

Dunstan Shekidele, Moro.

Toa comment