MAMA, BINTIYE WALIOPIGWA RISASI DAR UNDANI WA ANIKWA

MKAZI wa Tu­wamoyo, Kig­amboni jijini Dar, Halima Ibrahim ‘54’ na binti yake, Neema Andrea ‘24’ walijeruhiwa kwa risasi Jumatano iliyopita na binti huyo kupoteza maisha, Ijumaa Wikienda limechimba na kukuletea undani zaidi wa tukio hilo.  

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mwanahabari wetu alifunga safari hadi eneo lilipotokea tukio hilo na kuzungumza na ndugu pamoja na shuhuda wa tukio hilo.

 

Akizungumza na mwandishi wetu nyumbani hapo lilipo­tokea tukio hilo, mtoto wa mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Nuru Mohammed ‘35’ alisema: “Siku ya tukio nilikuwa nyumbani kwangu Maweni hapa Kigamboni, mida kama ya saa nne asubuhi, mama alinipigia simu na kuniam­bia yeye na mdogo wangu Neema wamepigwa risasi na hali zao ni mbaya hivyo nili­wahi haraka maana walikuwa bado hawajapata msaada wowote.

 

“Taarifa hiyo ilinishtua sana ambapo ndani ya dakika chache niliweza kutoka ninapoishi na kufika nyum­bani kwa mama ambapo niliwakuta wakiwa wamezun­gukwa na watu wakiwemo majirani. “Roho iliniuma sana nilipomuangalia mdogo wangu Neema ambaye alikuwa akilia na kunionesha jeraha kubwa kwenye paja la kushoto ambalo lilikuwa likivuja damu nyingi,” alisema Nuru.

 

Akizidi kusimulia kwa uchungu, Nuru alisema mbali na mdogo wake Neema, mama yake naye alikuwa akitoka damu nyingi. “Mama naye alikuwa akivu­ja damu alipojeruhiwa naye ilikuwa paja la kulia alikuwa akilia huku akimuonea huruma mwanaye Neema. “Sikuwa na la kufanya zaidi ya kushirikiana na wasamar­ia wema kuwakimbiza hos­pitali ya wilaya Kigamboni iliyopo mita chache kutoka hapa nyumbani.

 

“Wakati huo mdogo wangu alikuwa akiendelea kuvuja damu nyingi ambapo tulip­owafikisha walianza kupewa huduma ya kwanza na wau­guzi walikuwa wakihangaika kuzuia damu isimtoke mdo­go wangu lakini walikuwa kama wamezidiwa ndipo wakaita gari la wagonjwa na kumkimbiza Hospital ya Muhimbili lakini kwa bahati mbaya akafia njiani,” alisema dada huyo wa marehemu.

 

Alisema kwa upande wa mama yake ambaye kidogo hali yake haikuwa mbaya kama Neema, wahudumu wa hospitali hiyo waliamua kumuwahisha kwa gari lingine la wagonjwa Hospitali ya Temeke ambapo anaendelea na matibabu. Nuru alizungumzia tukio hilo huku akimuonesha mwandishi wetu maeneo aliyowakuta majeruhi wakitapatapa kuomba msaada baada ya kujeruhiwa.

 

Baada ya kuzungumza na dada huyo, mwandishi wetu alizungumza na shuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Hamza Viduka ambaye naye alieleza namna alivyoshuhudia. “Mimi marehemu alikuwa ni rafiki yangu, hivyo siku ya tukio tulikuwa tunapiga stori na mama wa marehemu alikuwa akiendelea na shughuli zake lakini ghafla tulisikia kelele huku filimbi zikipigwa, tulipoangalia tukamuona askari magereza akimkimbiza jamaa na kuwaomba wananchi wamsaidie kumkamata.

 

“Wakiwa wanaendelea kufukuzana ghafla wakatokea askari wengine wawili na Bajaj nao wakaanza kumsaidia mwenzao kumkimbiza huyo mtuhumiwa, baadaye wakatokea tena askari wengine wawili wakiwa na pikipiki huku mmoja akibeba bunduki, nao wakaanza kumuunganishia huyo jamaa.

 

“Baada ya dakika chache askari wote tukawaona wanarudi na huyo jamaa walishamkamata kwa kuwa lilikuwa ni tukio la kushangaza, mimi nikawa naangalia nikiwa hapa nyumbani na kuwaona hao askari wakitaka kuingia ndani ya geti la mahakama ndipo tukasikia mshindo mkubwa wa risasi ambayo tayari ilishawapata mama na mwanaye sehemu ya paja.

 

“Ukweli nilipata hofu kubwa sana nilipoona wenzangu wamejeruhiwa tena wakati mimi na Neema tulikuwa tumeshikana mikono, yaani sikuamini macho yangu nikahisi nami nimejeruhiwa lakini nilipojikagua nikajikuta niko salama ndipo tukaanza kufanya harakati za kuwapigia simu ndugu na jamaa ili tuweze kusaidiana,” alisema shuhuda huyo. Kufutia tukio hilo, dada wa marehemu aliwaangushia lawama askari hao na kuwashutumu kwa uzembe waliofanya na kusababisha mauaji hayo.

 

“Wanatakiwa kuwa makini wanapokuwa kwenye kazi zao, wanasema askari mwenye bunduki alipakizwa nyuma kwenye pikipiki na mwenzake na hiyo bunduki wanasema aliibeba kama begi ndiyo maana hiyo risasi ilipochomoka ikaja moja kwa moja kwa raia wasiokuwa na hatia.

 

“Ninavyojua askari awapo na bunduki ni lazima mdomo wa bunduki utazamishwe juu au chini kuepuka madhara kama hayo, sasa yeye wanasema aliibeba kama begi. wanatakiwa kuwa makini.” Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema askari anayedaiwa kufanya tukio hilo tayari ameshakamatwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani

Stori: Richard Bukos, Ijumaa Wikienda

Aliyepasuliwa KICHWA Badala ya MGUU, Azimia Kila SAA “JPM Nisaidie”

Loading...

Toa comment