The House of Favourite Newspapers

Mambosasa Amkamata Mlemavu Anayedaiwa Kuwa Kinara wa Madawa

 

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata kijana mmoja ambaye ni mlemavu wa miguu anayedaiwa kuwa ni kinara wa biashara ya madawa ya kulevya jijini humo.

 

Akizungumza na wanahabari leo Februari 16, 2018 , Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo limefanikiwa pia kuwakamata watuhumiwa wengine wawili ambao ni dereva wa basi na kondakta wakituhumiwa kukutwa na bangi.

 

“Tumekamata kreti 491, ndoo mbili za ujazo wa lita 20 zikiwa zimejazwa bangi, baada ya kuendelea na uchunguzi tukakuta ndoo mbili zenye ujazo wa lita 10 zikiwa zote zimejazwa madawa ya kulevya aina ya bangi na walikuwa wameziweka kwenye buti la basi hilo.

 

“Watuhumiwa ambao wamekamatwa kwenye basi hilo ni Shaban Said (52) mkazi wa Manzese ambaye ni dereva wa basi hilo pia alikamatwa Omari Juma (27) yeye ni kondakta na mwisho alikamtwa Hashim Mohamed (42) watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa watafikishwa punde mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika,” alisema Mambosasa. 

 

Mambosasa aliendelea kutolea ufafanuzi sakati hilo kwa kumuinua kijana mmoja ambaye ni mlemavu wa miguu ambaye anadaiwa kuwa ndiye mmiliki wa mzigo huo wa bangi.

 

“Huyu ndiye mmiliki wa madawa haya, mnaweza kuona mtu wa kumuonea huruma ndiye anauwa Watanzania. Tunapambana na vita ya madawa ya kulevya lakini huyu comrade ndiye mfanyabiashara wa madawa hayo.

 

“Niseme kwamba, hakuna atakayeachwa kwa aina yoyote ile kuendelea kuvunja sheria, sisi hatuangalii mtu ila tunaangalia kitu anachokifanya na tutakwenda mbali zaidi kuchunguza kama mmiliki wa basi na yeye anaendelea kuruhusu mabasi yake kubeba madawa ya kulevya,”  alisema Mambosasa.

Comments are closed.