The House of Favourite Newspapers

Mamilioni ya Aliyepumulia Mashine Familia Yapasuka

hamadFAMILIA tatu zinazomuhusu mkazi wa Ukonga, Majumba- Sita jijini Dar, Hamad Awadhi aliyekuwa akiishi kwa kutumia mashine ya gesi ya kupumulia kufuatia mapafu kusinyaa, zimeingia kwenye mtafaruku wakati wa mazishi yake huku chanzo kikidaiwa kuwa mamilioni aliyokuwa akichangiwa.

 

Familia hizo ambazo ni upande wa baba wa marehemu ukiongozwa na baba mkubwa, Hamisi Mohammed, upande wa mkewe ukiongozwa na baba wa mkewe (babamkwe), Benet Kulekana na upande wa mama yake ukiongozwa na bibi mzaa mama, Mary Greyson.

 

Baada ya Hamad kufariki dunia Alhamisi iliyopita, familia hizo kila upande ulitaka kuweka msiba kwake ambapo mjane wa marehemu, Catherine Kulekana alisema haendi popote zaidi ya kuweka msiba huo nyumbani kwa wazazi wake, Ukonga Majumba-Sita jirani na nyumba aliyokuwa akiishi na Hamad.

 

Wanahabari wetu walifika nyumbani kwa mjane huyo na kukuta kikao kizito kilichozihusisha familia hizo ambapo kila upande ulikuwa ukisema wenyewe ndiyo wenye mamlaka na mwili wa marehemu.

 

Baada ya kikao hicho, wanahabari wetu walizungumza na pande zote ambapo baba mkubwa (Hamis) ambaye alisema alitumwa na baba mzazi kuuchukua msiba na kuupeleka Tabata kwa baba yake kwa kuwa wao ndiyo upande wa baba na ndiyo waliomlea tangu utotoni.

 

Upande wa mama wa marehemu ukiwakilishwa na bibi (Mary) alisema yeye ndiye mwenye mamlaka na msiba huo.

Wakati upande wa baba na mama ukisema hayo, upande wa mkewe ukiwakilishwa na babamkwe (Kulekana) nao ulikuja juu ukisema wao peke yao ndiyo waliokuwa wakihangaika na Hamad siku zote ikiwemo kumuuguza.

 

Kwa kugandamizia kauli hiyo babamkwe, mke wa marehemu alitoa karatasi aliyodai ni wosia ulioachwa na marehemu ambaye alikuwa akitamka maneno na babamkwe huyo alikuwa akiandika.

Alipoulizwa suala la mashahidi wa wosia huo, Kulekana alisema alikuwa kwenye harakati za kuwatafuta mashehe na mashahidi wengine, lakini kwa bahati mbaya Hamad aliaga dunia.

 

Wakati pande hizo zikilumbana, mmoja wa wanafamilia aliyeomba hifadhi ya jina alisema tatizo kubwa la balaa hilo ni mamilioni aliyokuwa akichangiwa Hamad na wasamaria wema.

 

Miongoni mwa waliomchangia Hamad ni Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ambalo lilimchangia shilingi milioni kumi, kanisa moja lililopo Yombo, waumini wa Dini ya Kiislam na taasisi nyingine, zilizosababisha michango hiyo kuwa sintofahamu ya nani apewe.

 

Hata hivyo, mchana wa Jumamosi iliyopita, mwili wa Hamad ulitolewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Mloganzila) na kufikishwa ukweni kwake kisha kupelekwa katika Makaburi ya Segerea kwa ajili ya mazishi.

STORI: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN, DAR

 

Comments are closed.