The House of Favourite Newspapers

Man Mo: Sikubadili Dini, Niliimba Gospel Nitoke Kisanii

KUPITIA ‘msoto’ katika muziki au fani yoyote ni jambo la kawaida, Maneno Mohamed ‘Man Mo’ ni mmoja wa wasanii wenye uwezo wa juu wa kuimba na kutunga, amefunguka jinsi anavyopata wakati mgumu ‘kutoboa’ katika tasnia ya Bongo Fleva.

 

Man Mo ambaye ni mtunzi wa nyimbo nyingi ukiwemo wa Nasimama wa mkongwe Judith Wambura ‘Lady JayDee’, amefunguka kuwa licha ya kuanza kazi muda mrefu lakini bado ameshindwa kufika alipopategemea.

 

“Mama yangu alikuwa ni msanii, nilijifunza mwanzo kabisa kutoka kwake, baadaye nikaanza kupata uzoefu kwa kujifunza kutoka kwa wasanii wakubwa akiwemo Ali Kiba aliyekuwa akikutana naye studio mara nyingi.

 

“Nilitoka kwetu Pwani kuja Dar kufanya muziki, lakini haikuwa rahisi, nikajikuta naangukia kwenye kazi za kiwandani ili kujiongezea kipato, baadaye nikapata bahati ya kuwa chini ya Sharobaro Records.

 

“Nikiwa Sharobaro Records nilirekodi nyimbo nyingi zikiwemo Binti wa Kibara na Binti wa Kimasai.”

 

Anaeleza kuwa upepo ulibadilika na mambo yalikuwa magumu, akapata meneja aliyemshawishi kuimba muziki wa dini ya Kikristo maarufu kama nyimbo za Injili au gospel, alikubali ushauri huo na kuufanyia kazi licha ya kuwa yeye hakuwa Mkristo.

Alipata mwitikio mzuri kwenye muziki wa Injili lakini kwa kuwa asili yake ni dini nyingine ya Kiislam, kuna baadhi ya ndugu na familia hawakukubaliana naye kuhusu uamuzi wa kuimba muziki wa Injili.

 

“Sikuwa nimebadili dini yangu wala sina mpango huo, niliamua kuimba muziki huo ili kujitangaza na nilipata ushirikiano mzuri kwa wenzangu akiwemo Madame Flora ambaye tulizunguka matamasha mengi pamoja nikiimba muziki wa Injili jukwaani,” anasema.

 

Anakiri kuwa baadaye alirejea kuimba Bongo Fleva kutokana na kufikia hatua kuona hakuwa na uwezo wa kupata mwendelezo wa kisanii upande aliokuwepo, na yupo chini ya Kampuni ya African Network Entertainment (ANE), akiwa ametoa nyimbo za Tike na Mapenzi Kazi.

 

“Muziki ni mgumu lakini bado nina ndoto ya kuwa msanii ‘simple’ kama Ali Kiba lakini mwenye muziki mzuri wa kibiashara kama Diamond Platnumz,” anamaliza kusema.

Na Mwandishi Wetu

 

Comments are closed.